Kiongozi wa Mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Abdalla Shaibu Kaim ametembelea mradi wa majisafi ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es salaam na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo uliotekelezwa eneo la Mwembebamia, kata ya Chamazi, Temeke unaonufaisha takribani kaya 300.
Akizungumza wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Temeke, Ndugu Kaim amesema ameridhishwa na namna mradi ulivyotekelezwa kwa kuwa umezingatia vigezo, sambamba na upatikanaji wa nyaraka muhimu za mradi.
"Mbio za mwenge Kitaifa zimepitia taarifa ya utekelezaji wa mradi na kukagua nyaraka muhimu na tumeridhika na utekelezaji wa mradi huu" alisema na kutoa pongezi kwa jitihada zinazofanywa na DAWASA.
"Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu katika utekelezaji wa mradi huu ambao utaondoa changamoto ya ukosefu wa maji salama kwa wananchi wa maeneo haya. Pia niwapongeze Wabunge, Wakuu wa Wilaya za Temeke, Ilala na Kigamboni pamoja na viongozi wote wa kata kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huu katika maeneo yao," ameeleza Ndugu Kaim.
"Pia niwapongeze Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutekeleza mradi huu ambao ni suluhu ya tatizo la maji kwa wakazi wa mtaa wa Mwembebamia.
Alisema, Serikali inatambua nia njema ya DAWASA katika kumtua mama ndoo ya maji kichwani." ameeleza Ndugu Kaim.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa mradi wa majisafi pembezoni mwa mkoa wa Dar es salaam umetekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10 na utakapokamilika utahudumia wananchi wa maeneo ya Temeke, Ilala na Kigamboni.
Ameongeza kuwa chanzo cha mradi ni tenki la mradi wa maji Kibamba - Kisarawe lenye ujazo wa lita milioni 6 ambapo mabomba ya ukubwa tofauti yamelazwa kwa umbali wa kilomita 338 katika Wilaya zote 3.
"DAWASA itaendelea na kazi ya kulaza mabomba ya usambaza maji kwa fedha za ndani ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma ya maji," ameeleza Ndugu Kiula.
Amebainisha kuwa, mpaka sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 94, ambapo jumla ya kaya 234 zimeunganishwa huduma ya maji. Akasema lengo ni kuongeza maunganisho ya maji ili kufikia wananchi wote.
"Maji yameshafika eneo hili la Mwembebamia na tunawauganishia wananchi kwa mkopo kwa muda wa miezi 6, na watalipa kidogo kidogo." ameeleza Ndugu Kingu.
Naye Diwani wa Kata ya Chamazi, Ndugu Lawrence Gama amesema kuwa awali katika eneo hilo hapakuwa na maji safi na salama. "Tulikuwa tunategemea maji kutoka kwa watu binafsi, lakini kupitia maji haya tutakuwa tumeondoa shida ya maji kwa wananchi wote". Alisema
Mkazi wa Mwembebamia Aziza Khalid ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuwatua wanawake ndoo kichwani kupitia mradi wa Mwembebami. Alisema awali walikuwa wakichota maji ya visima kwa bei kubwa na kuongeza kuwa mradi unatusaidia kupunguza makali ya maisha kwa kupata majk salama, karibu na makazi na kwa gharama nafuu.