Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt. Adolf Rutayuga leo tarehe 4 Mei,2023, Mkoani Morogoro, amefungua rasmi kikao kati ya NACTVET na Ujumbe kutoka Sekretarieti ya Ajira nchini.
Dkt. Rutayuga amesema kikao hicho kimelenga hasa katika masuala ya ajira ili kuwajengea uelewa mpana juu ya wahitimu wanaopita katika vyuo mbali mbali vinavyosimamiwa na NACTVET.
Ameongeza kuwa kikao hicho ni fursa ya kuwapa wajumbe wa Sekretariati ya Ajira vigezo vinavyotumika katika mfumo mzima kuanzia udahili, ufundishaji na ujifunzaji na upimaji wa wanavyuo na namna wanavyoweza kukidhi soko la ajira ili kuwasaidia katika utendaji kazi wao.
Amesisitiza namna ambavyo Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vimekuwa vikitoa wahitimu nchini kwa kuzingatia misingi ya ujuzi na umahiri ambao ni chachu katika maendeleo nchini.
Aidha, kikao hicho kimekuwa daraja ambapo washiriki kutoka Sekretarieti ya Ajira wamepata nafasi ya kupitishwa kwa njia ya mjadala na mawasilisho kutoka Kurugenzi nne za Baraza kuhusu kile kinachosimamiwa na kila Kurugenzi na Vitengo vya NACTVET ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu kazi na majukumu ya Baraza.
Kikao kazi hicho kimejumuisha pia Wakurugenzi na maafisa waandamizi kutoka NACTVET ambao wameshiriki kuyatolea maelezo masuala yaliyojitokeza kama hoja za msingi kwenye mawasilisho yao.
Kwa Upande wake, Katibu Msaidizi Miundombinu wa Sekretarieti ya Ajira Bi. Mtange Ugullum, amepongeza na kuishukuru NACTVET na washiriki wote kwa kuandaa kikao hicho.
Amesema juhudi za Baraza zimefanya kikao hicho kuwa chenye manufaa Zaidi kutokana na taarifa muhimu walizopata ambazo zimewapa uelewa wa mambo muhimu yatakayowasaidia katika utendaji wao.
Bi Mtange amesema NACTVET na Sekretaria ya Ajira ni taasisi zinazotekeleza majukumu yao kwa lengo la kujenga nchi na hivyo majadiliano ya leo yamekuwa yenye faida na yamewapa uelewa mzuri kuhusiana na Vyuo vya elimu ya ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Amelishukuru Baraza na kulitaka kuendeleza ushirikiano na Sekretarieti ya Ajira ili kwa pamoja waweze kupunguza changamoto mbalimbali katika soko la ajira.
Social Plugin