Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinatarajia kuanza ujenzi wa Kituo cha kisasa katika eneo la ekari 105 lililopo Bungo Kibaha katika Mkoa wa Pwani kuanzia mwezi Julai 2023.
Hayo yamesemwa na Prof. Deus Ngaruko ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu-OUT, alipotembelea maonesho ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Prof. Ngaruko amesema kwamba:
"OUT imejipanga kujenga kituo cha kisasa cha utafiti, uvumbuzi, ubunifu na ukarimu Bungo Kibaha kuanzia Julai 2023. Hii ni kutokana na mradi wa Mageuzi ya Uchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) unaofadhiliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lengo la kituo hicho ni kwa ajili ya kutoa wahitimu na watafiti ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kubuni, kuibua na kuanzisha ajira nyingi kwa jamii ya Watanzania na kisha kuchochea katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Tayari kazi ya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho inaendelea vizuri."
Prof. Ngaruko ameendelea kueleza kwamba katika kituo hicho kutajengwa mashamba darasa ya mazao ya kilimo na mifugo, mabwawa ya kufuga samaki, mabwawa ya kusafisha maji taka, machinjio ya kisasa, ufugaji wa nyuki, maabara za sayansi, maabara za utalii na ukarimu, hosteli, nyumba za watalii, zuu ya wanyama na mambo mengine mazuri na makubwa kwa maendeleo ya Watanzania.
Vilevile, Prof. Ngaruko ameongeza kwamba, wafanyakazi katika uwekezaji huo mkubwa watakuwa ni wanafunzi wa OUT wanaosoma programu za Astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada za Umahiri na Uzamivu. Sehemu kubwa ya vitu vitakavyotumika ndani ya kituo hicho ikiwemo chakula na mahitaji mengine yote yanatarajiwa kuzalishwa hapo hapo.
"Hakika, hii ndivyo namna OUT inavyotaka kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuhakikisha vyuo vikuu vinaandaa mitaala na mazingira ya kuzalisha wahitimu ambao watakuwa na uwezo wa kujitegemea kwa kuanzisha ajira kwao wenyewe na kwa wanajamii wote wa Tanzania." Alihitimisha Prof. Ngaruko ambaye pia ni mratibu Mkuu wa mradi wa HEET kwa OUT.