Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu akizungumza na Wafanyakazi wa Ofisi hiyo alipokuwa akifungua mafunzo kuhusu huduma na taratibu za uwasilishaji madai na Mafao yaliyoandaliwa na WCF Leo Mei 30, 2023 Jijini Dodoma.
Afisa utumishi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Susan Kimambo akipima presha baada ya mafunzo hayo ambayo yaliyoambatana na upimaji afya.
Afisa Mwandamizi Themistocles Rumboyo kutoka akitoa elimu Kwa wafanyakazi kuhusu Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi (WCF)
Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi wa ofisi hiyo juu ya majukumu yanayotekelezwa na mfuko huo.
Akizungumza Mei 30, 2023 jijini Dodoma kwenye mafunzo kuhusu huduma na taratibu za uwasilishaji madai na mafao yaliyotolewa na WCF yaliyoambatana na upimaji afya, Prof. Katundu amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wafanyakazi na kutoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amehimiza wafanyakazi kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Naye, Afisa Mwandamizi kutoka WCF, Themistocles Rumboyo, amebainisha faida za wafanyakazi kujiunga katika mfuko huo ikiwemo uhakika wa kuendelea kulipwa mafao kipindi chote cha maisha ikiwa atapata ulemavu ambao hamruhusu kurudi kazidi, kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza migogoro baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Awali, Mtaalamu wa afya kutoka Kituo cha Afya cha Makole, Dkt. Ainea Mtango amewaasa wafanyakazi kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.