SERIKALI KUENDELEA KUFANYA MABORESHO KWENYE SEKTA YA MISITU NA NYUKI .


SERIKALI imesema itaendelea kufanya maboresho mbalimbali kwenye Sekta ya Misitu na Nyuki ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho kwenye Sera, Sheria, Miongozo na Kanuni ili kuongeza ufanisi na mchango wa sekta hizo kwenye Pato la Taifa.

Kiongozi wa ziara ya Mafunzo ya Utekelezaji wa Sera ya Misitu na Sera ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Msoffe amesema hayo wakati wa mafunzo ya Wadau wa Sekta za Misitu pamoja na Nyuki katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na kilwa na ambapo amewataka wadau hao wayatumie mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya yenye kuongeza mchango kwenye uchumi wa nchi.

“Tumekamilisha mafunzo ya kutoa elimu na kuangalia maeneo ambayo kisera, kisheria, kimuongozo na kikanuni yapo lakini hayafanyi vizuri Kuna mambo mengi ambayo tumeyaona yanahitaji maboresho, kurudiwa ama kubadilishwa kabisa ili kuendana na hali halisi ya ndani”

Kwa upande wake Mkazi wa Kilwa Masoko, Hashim Hassan ameipongeza TFS kwa kuwapa elimu ya Ufugaji nyuki ambayo imewaongezea kipato huku Mwanaidi Issa ambaye ni Mdau wa Misitu Wilayani Kilwa akiishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mafunzo hayo ikizingatiwa kuwa kwa sasa mazao ya misitu yamesaidia kubadilisha maisha yao na kuwawezesha kununua usafiri, kuweka mifumo ya umeme wa jua na kujenga Zahanati.

"Tunaishukuru sana Serikali kwa kututhamini na kutujali kwani elimu hii tunayoipata tutaisambaza kwa wenzetu ambao hawajapata bahati ya kushiriki mafunzo haya" amesema Mwanaidi

Aidha, ameongeza kuwa kitendo cha Wizara kuendelea kuwapatia mafunzo kinawaongezea elimu ambayo inawasaidia kufanya vizuri zaidi katika sekta hiyo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post