Serikali imesema itaendelea kuimarisha Sekta ya Anga ikiwemo kujenga viwanja vya ndege na kuboresha vilivyopo ili kuweza kuruhusu ndege kutua wakati wowote.
Akizungumza Mhe. Prof. Makame Mbarawa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wakati wa uwasilishaji wa bajeti yake ya mwaka 2023/24 amesema ili kuliwezesha Shirika la Ndege Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, Serikali itaendelea kununua ndege, kujenga viwanja vipya na kuboresha vilivyopo kuweza kuruhusu ndege kutua wakati wowote.
Amefafanua kuwa mwishoni mwa mwezi huu, watapokea ndege ya mizigo na mwezi wa nane wanakusudia kupokea ndege za abiria.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema viwanja vya ndege haviwezi kuwa na tija kama huna ndege. Mkakati wa ATCL ni kuongeza ndege ambapo wanatarajia mwezi huu mwishoni ndege ya mizigo na kabla ya Desemba 2023 kuongeza ndege mbili za masafa ya kati.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu (PAC) Mhe. Nahenjwa Kayoboka akichangia wakati wa bajeti hiyo wamesema Serikali iangalie uwezekano wa kurudisha umiliki wa ndege hizo kwa ATCL ili Kampuni iweze kujiendesha kibiashara kwa sababu kuna athari za kiutendaji na kimikataba ya Kimataifa kwa kuendelea kupuuzia madeni ya ATCL pamoja na umiliki wa ndege ambao unazalisha madeni makubwa yasiyo na tija na kusababisha hesabu za Kampuni kuonesha hasara kila mwaka.
Social Plugin