Na Mwandishi Wetu-MOROGORO
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imesema itaendeea kuwezesha uwepo wa majukwaa ya wafanyakazi ili kuhakikisha yanatoa nafasi ya wafanyakazi kujadili masuala yao.
Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri chini ya Ofisi hiyo, Pendo Berege ameyasema hayo Mei 17, 2023 katika mafunzo ya watendaji wa vyama vya wafanyakazi, waajiri na Shirikisho la vyama hivyo yaliyofanyika mkoani Morogoro yaliyolenga kukumbushana wajibu na majukumu katika utekelezaji wa katiba na kanuni za vyama.
Amesema ataendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha vyama hivyo vinatekeleza majukumu kwa weledi na bila kuingiliwa na kuwa majukwaa ya kujadili mambo yao.
Amesema katika sherehe za Mei Mosi serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ilielekeza vyama vya wafanyakazi kuhakikisha vinawasilisha masuala ya wafanyakazi serikalini hivyo majukwaa hayo ni kiunganishia ycha kushughulikia maslahi ya wafanyakazi.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya ametoa rai kwa Msajili wa vyama hivyo kuwasilisha ombi la ada ya uwakala serikalini isiingiliwe na watu serikalini ili kuondoa changamoto zinazojitokeza.
Social Plugin