MRADI WA KUBORESHA MIJI 45 (TACTIC) KUANZA MWEZI AGOSTI


Uboreshaji wa Miundombinu katika miji 12 kati 45 ambayo inanufaika na mradi wa TACTIC unatarajiwa kuanza Agosti, 2023 kufuatia Benki ya Dunia (WB) kuridhia kutoa Dola za Kimarekani milioni 410 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hayo yamebainishwa wakati  Wajumbe wa Bodi za Zabuni za halmashauri 12 mkoani Tanga ambazo ziko katika awamu ya kwanza ya mradi huo kukutana kujadiliana na kupewa mafunzo kuhusu utekelezaji wake.

Mratibu Msaidizi wa Miradi ya TACTIC, Mhandisi Emmanuel Manyanga amesema mradi unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa masharti nafuu wa benki ya dunia.

“Mwezi Julai wasimamizi wataingia katika maeneo ya miradi kwa ajili ya kupata takwimu za awali na mwezi wa Agosti wakandarasi wataingia na kuanza ujenzi kwa awamu hiyo,” amesema Manyanga.

Pia, Manyanga amesema mradi huo unaratibiwa na Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na kutekelezwa na Halmashauri za Miji 45 nchini.

Manyanga amesema Miji hiyo imegawanywa katika makundi matatu. Kundi la kwanza litakaloanza mradi huo linahusisha miji 12 ambayo ni Arusha, Dodoma, Geita, Ilemela, Kahama, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Songea, Sumbawanga na Tabora. 

Kundi la pili ni lenye miji 15 ambayo ni Babati, Bariadi, Bukoba, Iringa, Kibaha, Korogwe, Lindi, Moshi, Mpanda, Mtwara, Musoma, Njombe, Singida, Shinyanga na Tanga,” alisema Manyaga.

Bagamoyo, Bunda, Chato, Handeni, Ifakara, Kasulu, Kondoa, Mafinga, Makambako, Masasi, Mbinga, Mbulu, Nanyamba, Newala, Nzega, Tunduma, Tarime na Vwawa ni miji 18 ilipo katika kundi la tatu.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuanza kwa utekelezaji wa miradi hii ya TACTIC ambayo imesambaa karibu nchi nzima yenye lengo la kuboresha miundombinu ya miji na kuzijengea uwezo halmashauri ambazo zitatekeleza miradi hii,” alisema.

Amesema wameanza utekelezaji baada ya kutimiza matakwa yote ambayo walipewa na benki ya Dunia huku akisema kuwa awamu ya kwanza usanifu umeshakamilika na zabuni zimeshatangazwa na sasa wako katika hatua za mwisho kupata wakandarasi na wasimamizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post