Seattle, Washington State, Marekani
Serikali ya Tanzania imeeleza azma yake ya kuongeza juhudi za kutangaza utalii kupitia michezo pia kushirikiana na taasisi mbalimbali duniani ili kuongeza idadi ya watalii kutoka nje na mapato zaidi kwa Serikali.
Azma hiyo imeelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mei 5, 2023, wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya Vulcan kwenye Uwanja wa Lumen jijini Washington nchini Marekani na kushirikisha wadau kutoka makampuni mbalimbali yaliyoko jijini Seattle ikiwemo wawakilishi kutoka Google, Starbucks, ofisi ya Meya wa Seattle, Boeing na jumuiya ya wafanyabiashara.
Taasisi ya Vulcan inamiliki hisa katika klabu kubwa za michezo mbalimbali katika ligi kuu za nchini Marekani za Seattle Sounders (mpira wa miguu); Seahawks (soka la Marekani) na Portland Trailblazers (Ligi ya NBA).
“Nimewahi kufika Tanzania, naweza kuwahakikishia kuwa kwa wale ambao hawajafika mfike ni nchi nzuri sana. Tuliwahi kwenda pia Sounders miaka ya 2000 ikacheza na Yanga, Simba na Timu ya Taifa,” alisema Bw. Adrian Hanauer, ambaye kwa sasa ni mmiliki mwenye hisa nyingi wa klabu ya Seattle Sounders akiahidi klabu hiyo na wadau wengine wako tayari kushirikiana kusukuma mbele utalii wa Tanzania.
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) chini ya Mtendaji wake Mkuu, Damasi Mfugale, imeingia makubaliano ya awali kuelekea ushirikiano kamili na makampuni ya Vulcan.
Social Plugin