Katika kupambana na vitendo vya ugaidi na utakatishaji fedha haramu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imezindua mwongozo wa ushirikiano wa wadau katika upelelezi, uratibu na kupambana na makosa hayo.
Akizungumza mara baada ya uzinduzia wa mwongozo huo uliofanyika Jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria amesema kuwa mwongozo huo utasaidia kuleta pamoja wadau wanaopambana na makosa hayo na hivyo kukomesha uhalifu huo.
“Kila mmoja amekuwa akifanya kivyake vyake, lakini kwa mwongozo huu unawaleta pamoja wadau wote ili juhudi zao za kudhibiti makosa haya matatu ya utakatishaji wa fedha, ufadhili wa ugaidi na ugaidi wenyewe uweze kufanyika kwa pamoja maana tunafahamu umoja ni nguvu,” amesema Waziri Ndumbaro.
Dk. Ndumbaro ameongeza pia kuwa mwongozo huo hautaunganisha wadau wa ndani ya nchi pekee bali pia unatoa mwongozo wa namna ya kushirikiana na nchi nyingine Duniani kukabiliana na makosa hayo.
“Mtu anaweza akafanya uhalifu wa ugaidi au utakatishaji fedha akajipatia fedha na kuwekeza kwenye nchi nyingine,” amesema Waziri Ndumbaro huku akitoa wito kwa jamii kuwafichua wanaoshiriki vitendo hivyo katika jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Sylvester Mwakitalu amesema mwongozo huo ni muhimu na utasaidia taasisi za uchunguzi kukusanya taarifa za uhalifu kwa kushirkiana na kuwasaidia kuendesha mashtaka ya makosa hayo.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo,Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CP. Salum Hamduni na wadau wengine kutoka ndani na nje ya nchi.
Social Plugin