SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kaskazini limeweza kutoa jumla ya vyeti na leseni 113 za uthibitisho wa ubora na usalama wa bidhaa kwa wazalishaji 82, ambapo hamsini na nne (54) ni wajasiriamali wadogo.
Aidha, kati ya vyeti na leseni 113 zilizotolewa, vyeti na leseni 73 sawa na asilimia 64.6% zilitolewa kwa wajasiriamali wadogo. Vyeti na leseni hizo zinahusisha bidhaa mbalimbali za vyakula, vipodozi, vifaa vya ujenzi, vilainishi, bidhaa za ngozi na vifungashio
Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililofanyika mkoani Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongela amesema wanampongeza Rais Samia kwa kuendelea kulipia gharama za kuwahudumia wajasiriamali wadogo katika ukaguzi na upimaji wa bidhaa zao pasipo wao kulipia gharama hizo ambapo kwa kipindi husika jumla ya Tshs. 182,500,000/= zimetumika katika kuwahudumia hao wajasiriamali wadogo 54
Aidha RC Mongela amesema TBS Kanda ya Kaskazini imekwisha sajili majengo mia sita sitini (660) ya biashara na ya kuhifadhia bidhaa za vyakula na vipodozi.
"Niwaombe wafanyabiashara mbalimbali katika Kanda ya Kaskazini kutoa ushirikiano kwa TBS ili kuwezesha soko letu kuwa na bidhaa za chakula na vipodozi bora na salama ili kuleta tija inayotarajiwa". Amesema
Pamoja na hayo amesema kuwa, kwa upande wa eneo la ujenzi wa maabara hapa Arusha, Serikali ya Mkoa itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kwamba maabara ya TBS inajengwa katika mazingira yatakayoleta tija kwa Taifa.
Hata hivyo amewataka wazalishaji hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri kwa wazalishaji wengine ambao bado hawajathibitisha ubora wa bidhaa zao, lengo likiwa ni kuwa na soko lenye bidhaa bora kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS) Bw. Lazaro Msasalaga amesema Vyeti na leseni ambazo zimekabidhiwa kwa wazalishaji vitasaidia bidhaa zilizothibitishwa ubora wake katika kuongeza imani kwa umma, kukubalika sokoni, kupata faida ya kiushindani sokoni (competitive advantage) na kuingia na kuuza bidhaa hizo katika soko la Afrika Mashariki pasipo kukaguliwa na kupimwa tena.
"Hii inatokana na kazi kubwa iliyofanyika ya uwianishaji wa viwango na mifumo ya uthibiti na udhibiti katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.". Amesema