TGNP YAKUTANISHA WANAUME MSALALA KUZUIA UKATILI WA KIJINSIA



Na Mwandishi Wetu, Msalala
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeendesha mdahalo wa kutomokeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto katika Kata za Lunguya na Msalala, Halmashauri ya wilaya ya Msalala,wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.

Mdahalo huo uliowahusisha wanaume, pia wameshiriki wanaume ambao ni viongozi wa kijamii, kama wazee wa mila, wakango na Viongozi wa Dini, ili kuwapa nafasi wanaume kujadiliana wenyewe nafasi yao katika kutokomeza, kuzuia na kuwalinda watoto wa kike dhidi ya Ukatili ikiwa ni pamoja na kutokomeza mila na destru inazochangia vitendo hivyo.

Katika mdahalo huo, pia wanaume hao walipendekeza kushirikiana na serikali kujenga mazingira salama kwa watoto wanaosoma shule za sekondari kwa kuhakikisha wanajenga mabweni ya wasichana ili kuwakinga na hatari ya kupata ujauzito kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.

Akizungumza Mtendaji Kata wa Shilela Mwanaidi Mzee, wakati wa mdahalo huo, alisema kwamba kupitia Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Msalala, Kata hiyo imepatiwa sh. Milioni 10 kwaajili ya kuanza ujenzi wa bweni la wasichana, ambapo ushiriki wa jamii yote kwa ujumla ni muhimu sana ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kuwa na tija.


“Tumekubaliana, fedha hii iliyoingia, tuanze ujenzi mara moja maana tunahitaji kuweka mazingira salama kwa watoto wa kike wanaosoma katika shule hii, ni muhimu sana. Tunahitaji nguvu kazi ya kutosha ili tumalize kwa wakati’ alisema Mwanaidi.

Kwa upande wa kata ya Lunguya wanaume walioshiriki mdahalo huo, walikubaliana kwamba, kwa pamoja warudi kwenye mila nzuri za kulea vijana ili kujenga kizazi chenye maadili kwani maadili yameharibika sana miongoni mwa jamii.

Aidha walikubaliana kwamba wanaume warudi kwenye nafasi yao ya kusimamia watoto na kuwajibika kwani endapo wanaume wataendelea kuwaachia wanawake kusimamia familia, na kulea watoto tatizo la ukosefu wa maadili litaendelea katika jamii na mimba za utotoni hazitapungua.


Pia wameshauri serikali za vijiji kuweka sheria ndogo za kuzuia watoto wa shule wa kike na kiume kushiriki kwenye ngoma za usiku, sherehe na kuzurura hovyo mitaani usiku, ili kuwaepusha na vishawishi.

Washiriki wameshauri pia, jamii kurudisha utamaduni wa asili wa kufanya vikao vya familia (vikome) kati ya Baba na watoto ili kujenga maadili mema, na kukemea tabia chafu ikiwa ni pamoja na kujenga uwajibikaji katika familia.


“Turudishe utamaduni wa asili, vikao vyetu vya Baba wa familia na watoto vilikuwa na maana sana wakati ule, tumekimbilia tamaduni za nje, umesahau mamabo yetu. Vikome vilisaidia sana kujenga maadili. Wazee w a leo, wamekuwa hivyo kwa sababu ya vikao vya familia (vikome) siku hizi hakuna”, alisema Mchungaji Joseph Mwamashimba.

Mwezeshaji wqa Midahalo huo kutoa TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, mdahalo huo ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa mataifa la idadi ya watu (UNFPA), na Shirika la Msaada wa Korea (KOICA), ambao unalenga kubadilisha mitazamo, mila na destru kandamizi zinazochangia Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post