Na John Mapepele.
Serikali imesema hakuna mwananchi aliyenyanyaswa kijinsia, wala mifugo ya mwananchi yeyote (Ng’ombe 250) kuporwa au taarifa ya mtu yeyote kutaka kujinyonga pia hakuna uthibitisho wa vitendo vya wanawake kuvuliwa nguo na Askari wa Uhifadhi katika tukio la Askari wa TANAPA kuwaondoa ndani ya Hifadhi ya Ruaha Wananchi watano (5) wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya kama ilivyoelezwa hivi karibuni Bungeni na Mbunge wa jimbo hilo wakati alipoomba Mwongozo kwa Mhe. Spika akiomba Bunge lihairishe mjadala ili kujadili suala hilo kama dharura.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali bungeni leo Mei 15, 2023 kuhusu tukio hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema ni kweli kuwa Mei 6 mwaka huu, Askari wa TANAPA wakiwa katika doria za kawaida walifika katika Kijiji cha Mwanavala na helikopta katika maeneo yaliyopo ndani ya Hifadhi ya RUAHA ambapo ni sawasawa na KM 20 ndani ya hifadhi ya TANAPA kutoka ulipo mpaka ambalo ni eneo la hifadhi lisiloruhusiwa Wananchi kuingia kwa kuwa ni karibu na Mto RUAHA ambao ni sehemu ya chanzo cha kupeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Ameongeza kuwa Askari husika wakiwa katika doria za kawaida walibaini ujenzi wa maboma mawili mapya ya mifugo ndani ya hifadhi ya RUAHA kinyume cha Sheria ambapo katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa, Wananchi hawa, waliongia kijinai na kinyume cha Sheria katika eneo la Hifadhi walizuia kutiwa nguvuni kwa kurusha mawe, fimbo, mishale na silaha nyingine za jadi na kusakizia mbwa askari wa Jeshi la Uhifadhi kwa lengo la kuwadhuru askari hao.
“Miongoni mwa silaha za jadi zilizorushwa zilitishia usalama wa Askari Jeshi la Uhifadhi waliokuwa katika kazi yao halali ya uhifadhi na kupelekea kitako cha bunduki aliyokuwa nayo askari kuvunjika. Nguvu waliyotumia askari kujilinda ilipelekea majeraha kwa Wananchi hao na askari Jeshi kulazimika kuwadhuru mbwa waliowasakizia kwa hofu ya kulinda maisha yao.” Amesisitiza Mhe.Mchengerwa
Ameongeza kuwa baada ya mivutano hiyo Wananchi wote waliopata majeraha walipelekwa hospitali na walipatiwa matibabu ambayo yaligharamiwa na TANAPA na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida pamoja na kwamba tukio husika limetokea ndani ya hifadhi, Wizara iliona ni busara kutoa pole ya shilingi milioni moja kwa kila mwananchi aliyeathirika na tukio hilo.
“Ikumbukwe mbele ya Bunge lako tukufu kuwa eneo lilipotokea tukio hili ni karibu na eneo yalipotokea mauaji ya Askari wa Uhifadhi Ndugu Yusti Matei na askari wa Wanyamapori wa Vijiji Ndugu Isaya Mwambe miaka michache iliyopita.
Takwimu za Wizara zinaonesha kwamba Askari wa Jeshi la Uhifadhi 15 wameuwa na wengine 51 wamejeruhiwa na Wananchi wavamizi ndani ya Hifadhi mbalimbali nchini wakiwa wanatekeleza majukumu yao.” Amefafanua, Mhe. Mchengerwa
Aidha, Mhe.Mchengerwa amesema Askari wote waliohusika na tukio hilo waliandikishwa maelezo Polisi kufuatia maelekezo ya Serikali na maelekezo yake. Kufuatia tukio liliojitokeza Wilayani Mbarali Serikali imetoa maelekezo sita.
Akisoma maelekezo hayo Mhe. Mchengerwa amesema Askari wote wa uhifadhi nchini watumie weledi wao katika kudhibiti uvamizi kwenye hifadhi badala ya kutumia nguvu kupita kiasi katika utekelezaji wa himasheria, ambapo amesisitiza kuwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya Sheria ili Sheria ichukue mkondo wake.
Aidha amesema tukio la Mbarali limetokea ndani ya Hifadhi ya Ruaha takriban kilomita10 baada ya mpaka mpya wa hifadhi na kilomita 20 ndani ya mpaka wa zamani karibu kabisa na Mto Ruaha ambao ndio mto tegemezi unaozalisha maji yanayotegemewa katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo Serikali kupitia kodi za wananchi inatumia zaidi ya Trilioni 6.5 kulijenga, lakini pia ndio mto tegemezi wa maji ya kunywa lakini na chanzo cha maji katika mito mbalimbali nchini.
“Hii inadhihirisha kwamba wananchi hao waliingia ndani ya hifadhi kimakosa, bila kufuata taratibu za kisheria. Eneo hili halina ruhusa ya kulima wala kufuga, wala mapito ya wananchi na hii ni kwa kuzingatia hali halisi ya uwandani kama nilivyoeleza hapo juu sambamba na kulinda maeneo oevu ili mito iweze kurejesha mikondo yake ya asili ya mitiririko yake ya maji kama nilivyoeleza.” Ameelezea Mhe. Waziri.
Amewasihi wananchi kufuata sheria na taratibu zote za maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kwa maslahi ya watanzania wote kwa ujumla wa vizazi vya sasa na baadaye pia ameendelea kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, kusaidia katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa maeneo haya yaliyohifadhiwa.
Amewataka Wahifadhi wote nchini kuwawashirikisha viongozi wa Chama na Serikali katika kutatua migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi ikiwemo kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo; lakini watambue kwamba wananchi ni wahifadhi namba moja hivyo waboreshe mahusiano baina yao na wahifadhi wananchi na kila kiongozi wa uhifadhi katika eneo lake atapimwa kwa namna anavyoshirikiana na wananchi katika maeneo yao ambapo amesisitiza wakaimarishe mahusiano yao na wananchi na vijiji vinavyopakana na hifadhi.
Pia Wahifadhi wote nchini waendelee kuimarisha doria, kuweka alama za mipaka, kuweka mabango na kulima mkuza ili kudhibiti uvamizi katika maeneo ya hifadhi kwa mustakabali wa nchi yetu ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo, kufua umeme na kilimo hususan programu za umwagiliaji.
Ameiagiza TANAPA kuanza ujenzi wa Rangers Post (kituo cha Askari wa Uhifadhi) ili kuimarisha ulinzi katika eneo la Hifadhi ya Ruaha Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amesema katika kupata suluhisho la kudumu la migogoro katika hifadhi hii kongwe iliyoanzishwa mwaka 1910 iliyojulikana kwa jina la hifadhi ya Saba, mwaka 1946 ilibadilishwa jina na kuitwa RUNGWA na mwaka 1964 Mwalimu Nyerere aliporidhia iitwe RUAHA, Serikali inakusudia kumega eneo la hifadhi lenye ukubwa wa takribani hekta 34,000 ili zitumike kwa shughuli za maendeleo ya wananchi ambapo Wananchi wa Vijiji husika watajipangia mpango bora wa matumizi ya ardhi.
Aidha Serikali itaondoa ekari 900 ili zitumike kwa shughuli za malisho.
Wiki hii Serikali itakamilisha uthamini wa mali za wananchi katika baadhi ya maeneo ya Kijiji cha Mwanavala ili taratibu zingine za fidia ziendelee.
Vilevile napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imekamilisha uwekaji wa vigingi katika mpaka mpya wa hifadhi ya Ruaha.
Amesema kwa sasa Serikali inakamilisha mchakato wa kuandaa rasimu ya Tangazo la Serikali (Government Notice – GN) jipya la Hifadhi ya Taifa Ruaha na mara taratibu husika zitakapokamilika Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali italeta Azimio Bungeni ili kupata ridhaa ya Bunge kama ilivyo kwa mujibu wa sheria na hatimaye kuwasilishwa GN hiyo kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua stahiki.
Social Plugin