Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE,WADAU WA CHAI WATAKA SERIKALI KUMALIZA CHANGAMOTO KWENYE SEKTA YA CHAI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

Serikali imetakiwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji wa zao la Chai ili kuondokana na changamoto zinazosababisha kushuka kwa tija na ubora hafifu wa zao hilo nchini. 

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa bodi ya Chai nchini Mustapha Umande  amesema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Chai duniani ambayo kitaifa imefanyika Jijini Dodoma kwa kuwashirikisha wadau,wataalam na mitandao ya wanazuoni ili kubadilishana uzoefu wa mnyororo wa thamani. 

Amesema ikiwa zao la Chai litapewa kipaumbele na kuongezewa thamani itasaidia kuchagiza uzalishaji na masoko endelevu ya zao hilo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Pamoja na hayo amesema siku ya Chai duniani inasaidia kujenga ufahamu Kwa wadau wa kilimo hicho na kuhamasisha uzalishaji endelevu unaozingatia uhifadhi wa mazingira na kuibua fursa na kutatua changamoto. 

"Kupitia siku ya Chai duniani sisi wadau tunapata pia nafasi ya kutoa mapendekezo ya kiutendaji na ya kisera yatakayoboresha uzalishaji wa chai nchini,"amesema . 

Kutokana na hayo Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe amesema tayari Wizara  imefungua ofisi za umwagiliaji  katika wilaya 102 ili kuongeza uzalishaji wa chai kwani katika kipindi cha miaka 10 imekuwa kwa  hasi moja. 

Waziri Bashe amesema mwenendo wa ukuaji katika sekta hiyo haupo vizuri kwani katika kipindi cha miaka 10 imekuwa kwa hasi moja. 

Aidha ameiagiza bodi hiyo kuhakikisha ifikapo Julai mwaka huu  mnada wa biashara ya chai uanze   baada ya kuwa na danadana ya uanzishwaji wake huku akisisitiza hakutakuwa na athari za kibiashara. 

Kwa upande wake Naibu Waziri, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na biashara Exaud Kigalu amesema suala la changamoto zilizopo kwenye sekta ya Chai nchini zinatokana na baadhi ya wawekezaji kushindwa kuwalipa wakulima Kutokana na uchache wa Viwanda. 

Amesema "tunahamasisha wakulima kulima mbegu bora ili kupata mazao mengi na badala yake wakivuna hawana pa kupeleka,usindikaji wa chai imekuwa wa kusuasua,tunawapa mzigo hawa wazalishaji,ni jukumu letu kuwasaidia,"mesema 

Kigalu ambaye pia ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini amesema ni wajibu wa Serikali kuona namna ya kuhamasisha uwekezaji wa Viwanda vidogo ili kunusuru tasnia hiyo . 

"Kupitia adha hii wanayopata wakulima tuone namna ya kuwapunguzia wakulima baadhi ya Kodi zimazo waumiza Ili kufidia hasara wanayopata; 

Hata hivyo tunaendelea kutafuta masoko nje ya nchi kupitia balozi zetu na kuhamasisha unywaji wa chai kupitia Viwanda vyetu vya usindikaji,"amesema 

Amesema sekta nyingi zinategemea sekta ya Kilimo hivyo ni wazi kuwa ikiwezeshwa itasaidia nyingine kufanya vizuri. 

"Kwa  takwimu za mwezi wa nne mwaka huu,sekta tatu zimeongoza ambapo kwenye Uwekezaji zimetengenezwa ajira zaidi ya 15000, Usafirishaji ajira 1767 na Kilimo ajira 451 hii inamaanisha Kilimo kinategemewa na sekta zote,"amesema 

Naye Mkurugenz Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Mary Evarist amesema bodi hiyo inatambua uwepo wa changamoto ya kushuka kwa uzalishaji na ubovu wa chai kunakotokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara. 

Pia ameeleza kuwa ucheleweshaji wa malipo ya wakulima wadogo wadogo kwa baadhi ya Viwanda, uwekezaji mdogo kwenye tasnia ya Chai,bei ndogo na migogoro ya waendeshaji wa Viwanda. 

Kutokana na hayo amesema bodi imeandaa mkakati wa kufuta na kutibu changamoto zote hizo ili kuleta mapinduzi kwenye sekta hiyo Kwa kuongeza uzalishaji na kifufua mashamba , kuweka mazingira wezeshi, kushughulikia migogoro iliyopo na kuhamasisha uanzishwaji wa kusindika chai maalumu. 

Mkakati mwingine ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara kwenye mashamba ya chai na kuboresha utafiti wa mbegu bora zitakazozalisha chai nzuri.

Akichangia katika mkutano huo,Mbunge wa Njombe,Deo Mwanyika (CCM) amesema kubwa wanaloliomba kwa wizara ya kilimo ni chai wanayozalisha wakulima  iwe na tija na ubora. 

"Mimi natoka Njombe ndio inaongoza kwa kuwa na wakulima wadogo wadogo tuna kila sababu ya kuwasaidia hao wakulima, wanahitaji kuongeza uzalishaji,"amesema Mbunge huyo. 

Mbunge wa Muleba Kaskazini,Charles Mwijage (CCM)  amesema zao la chai sio la kodi bali linatakiwa kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi. 

"Wanaolima chai ni watu wa kipato cha chini kodi ya nini,"alisema Mbunge huyo ambaye amewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika awamu ya tano. 

Naye Mbunge wa Lupembe,Edwin Swale (CCM) amesema  kutokana na mfumo ulivyo chai  nyingi inapotea kabla ya kufika kiwandani kutokana na usafirishaji kuwa wa kiwango cha chini. 

Mbunge huyo ameiomba Serikali kupeleka maafisa ugani mashambani kwani baadhi ya wakulima wanalima bila kufuata taratibu hivyo kuzalisha chai ambayo haina ubora. 

"Tunaomba muwape nafasi watu wanaokuja Wizarani, Waziri na Katibu Mkuu tusaidieni ili tufungue ukurasa mpya,"alisema Mbunge huyo. 

Mbunge wa Kilolo,Lazaro Nyamoga (CCM) amesema kinachoiumiza sekta ya chai ni kutokana na wanahusika kutochukua maamuzi magumu kwenye sekta hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com