Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI WA SEKRETAIRIETI YA MAADILI WAPIGWA MSASA KATIKA MASUALA YA UCHUNGUZI WA KIDIGITALI


Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akifungua mafunzo kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023 Jijini Arusha.
Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. John Kaole akitoa neno la utangulizi katika mafunzo kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023 Jijini Arusha.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya Pamoja na wakufunzi pamoja na washiriki wa mafunzo kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023 Jijini Arusha.

Na.Mwandishi Wetu-ARUSHA

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao ni wachunguzi wamepatiwa mafunzo kuhusu Uchunguzi wa fedha na uchunguzi wa kidigtali.

Akifungua mafunzo hayo leo Mei 8,2023 jijini Arusha Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeona ipo haja ya kuwapatia watumishi hao mafunzo hayo kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia katika maeneo mbalimbali kama vile biashara, mifumo ya fedha , na maeneo mengine ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wa Serikali na sekta nyingine .

Mhe. Kamishna alieleza kuwa kutokana na changamoto zilizobainika wakati wa utekelezaji wa baadhi ya majukumu ikiwepo suala la kufanya uchunguzi wa masuala ya fedha na uchunguzi wa kidigitali Sekretarieti ya Maadili imeona ipo haja ya kuwapatia watumishi wake mafunzo hayo ili kupata elimu ya uchunguzi wa kiteknolojia.”Tumeona kuwa ni lazima kujifunza na kuelewa namna ya kufanya kazi kulingana na mifumo hii ya kidigitali kadri inavyobadilika ili kupata matokeo mazuri hasa katika nyanja hii ya uchunguzi” alisema.

Aidha Mhe. Kamishna alisema kuwa matarajio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma katika mafunzo hayo ni kuwapata watumishi ambao wataweza kuwa wakufunzi watakaoweza kuwafundisha watumishi wengine namna ya kufanya uchunguzi wa kifedha pamoja na uchunguzi wa kidigitali katika kukusanya taarifa zinazotokana uchunguzi mbalimbali.”Tumewaleteni nyie wachache ili mkawe waalimu kwa watumishi wengine ambao hawapo hapa” alisema .

Awali akielezea majukumu ya Sektetarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Bw, John Kaole alisema kuwa pamoja na majukumu megine Sektetarieti ya Maadili ina jukumu la kupokea fomu za tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni ya viongozi wa umma na kufanya uchunguzi wa awali wa ukiukwaji wa maadili ambao hubainisha kama kuna vihatarishi vyovyote vya ukiukwaji wa Maadili.”Tunafanya uchunguzi wa awali kwa Viongozi wa Umma na endapo tukibaini kuwa kuna ukiukwaji wa maadili tunawapeleka katika Baraza la Maadili kwa ajili ya uchunguzi wa kina,” alisema.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Afisa Uchunguzi Mwandamizi kutoka Makao Makuu Dodoma Bw. Gideon Mafwiri alisema kuwa watumishi hao wamekua na changamoto ya kukosa weledi wa kutosha katika uchunguzi wa masuala ya fedha na uchunguzi wa kidigitali iliyopekelea kushindwa kupata taarifa sahihi katika uchunguzi wa masuala ya fedha na kidigitali” Tumekutana na baadhi ya viongozi wa umma hususan wafanyabiashara kuendesha biashara zao kimtandao na sisi hatukuwa na uweledi wa kutosha katika eneo hili la uchunguzi hivyo baada ya mafunzo haya ni imani yetu kwamba tutakuwa na weledi wa kutosha katika maeneo hayo,”alisema.

Mafunzo hayo ya siku tano kwa watumishi hao yaliongozwa na waratibu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka Makao Makuu Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com