WAZIRI DKT MABULA ATAKA WANANCHI TARIME KUACHA KUISHI KWA MAZOEA NA KUFUATA SHERIA

Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee (wa pili kushoto) akiwaonesha Mawaziri Dkt Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (wa tatu kushoto), Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki (wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Maliasili Mary Masanja (wan ne kushoto) wakati mawaziri hao walipofanya ziara wilayani Tarime tarehe 6 Mei 2023.


****************

Na Munir Shemweta, WANMM TARIME

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi wa Kegonga na Karakatonga wilayani Tarime mkoa wa Mara kuacha kuishi kwa mazoea na kufuata sheria ili kuepuka migogoro baina ya vijiji hivyo na maeneo ya hifadhi.

Dkt Mabula amesema hayo tarehe 6 Mei 2023 katika kijiji cha Kegonga kitongoji cha Lisolya kata ya Nyanungu wilayani Tarime, wakati timu ya mawaziri watatu ilipotembelea eneo hilo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa kuwataka mawaziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kwenye wilaya za Tarime na Serengeti mkoani Mara.

Mawaziri waliotembelea vijiji hivyo ni Angellah Kairuki, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula pamoja na na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Mary Masanja.

Vijiji vilivyopo kwenye mgogoro na eneo la Hifadhi ya Serengeti wilayani Tarime mkoa wa Mara ni Kegonga, Nyandage, Masanga, Karakatonga, Gobaso, Nyabirongo pamoja na Kenyamosabi.

Dkt Mabula amewaambia wananchi wa vijiji hivyo kuwa, kitendo cha timu ya mawaziti watatu kwenda eneo la mpaka lenye mgogoro ni ishara kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amewaheshimu wananchi wa maeneo hayo.

‘’Hivi ni vijiji vingapi tumekwenda mpaka kwenye alama za mpaka (Beacon), mnakaa mezani mnasoma then watu wanajua hapa ni pale lakini hapa tumekuwa akina tomaso tumekuja hadi hapa lakini hilo hamlioni kama Mhe. Rais amewaheshimu sana, ndugu zangu hebu tuache kuishi kwa mazoea tufuate sheria’’ alisema Dkt Mabula.

Amewataka wananchi wa mkoa wa Mara kuacha ubishi na kufuata sheria huku akiwatahadharisha dhidi ya watu wanaokwenda kuwadanganya na kueleza watu hao wana lengo la kutafuta kura wakati wa uchaguzi na kueleza kuwa iwapo wataishi kwa kukubali kudanganywa waelewe kuwa mpaka baina ya vijiji hivyo na hifadhi utaendelea kubaki kama ulivyo.

Amewaomba wananchi wa vijiji hivyo kuheshimu kile ambacho kipo kwa mujibu wa sheria na kueleza kuwa GN 265 ya mwaka 1968 ambayo wao wanaitambua ndiyo iliyotafsiriwa na si vinginevyo na kuhoji wanachoshangaa ni kitu gani.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, eneo la ukingo yaani Buffer zone la mita 500 ambalo Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassana ameridhia kuachiwa vijiji husika katika eneo hilo ambapo ameagiza kufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia wataalamu.

Amewaonya wananchi wa maeneo yenye mgogoro na hifadhi kuwa kwa kuwaeleza kuwa, iwapo wataendelea kubishana kuhusiana na mpaka kila siku basi hakutakuwa na maendeleo na kusisitiza kwamba ni vizuri kuacha kufanya kazi kwa mabishano.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, tafsiri sahihi kuhusiana na alama ya mpaka imetolewa na kusisitiza kuwa alama hiyo inapaswa kuheshimiwa ingawa baadhi ya wananchi wanaweza kuuma lakini hiyo ndiyo tafsiri sahihi iliyosomwa neno kwa neno na kuweka wazi kuwa, kinachotakiwa ni kutokuwa na ubishi na kukubali uanzishwaji wa hifadhi na mipaka iliyowekwa sambamba na ile inayoenda kubadilika.

Serikali kupitia wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka jumla ya alama 176 za mipaka katikati ya Alama Kuu Nane zilizotangazwa kupitia GN 235 ya mwaka 1968 ili alama za mipaka ziweze kuonekana vizuri kwa wananchi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati aliyevaa miwani) akiwaongoza mawaziri wenzake kuangalia ramani wakati walipotembelea eneo lenye mgogoro la Kegonga wilayani Tarime mkoa wa Mara tarehe 6 Mei 2023.
Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula (wa tatu kulia), Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki (wa tatu kushoto), Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mary Masanja (wa pili kushoto), Mbunge wa jimbo la Tarime Mwita Waitara (wa kwanza kulia) wakielekea kukagua alama ya mpaka katika kijiji cha Kegonga wilayani Tarime mkoa wa Mara.
Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula akielekea kijiji cha Kegonga kitongoji cha Lisolya kata ya Nyanungu wilayani Tarime mkoa wa Mara wakati timu ya mawaziri watatu ilipokwenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka katika eneo hilo tarehe 6 Mei 2023.
Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki wakitoka kukagua alama ya mpaka katika kijiji cha Kegonga kitongoji cha Lisolya kata ya Nyanungu wilayani Tarime mkoa wa Mara wakati timu ya mawaziri watatu ilipokwenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka katika eneo hilo Mei 6, 2023.
Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee wakiangalia muelekeo wa mpaka katika kijiji cha Kegonga wilayani Tarime mkoa wa Mara wakati timu ya mawaziri watatu ilipokwenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka katika eneo hilo tarehe 6 Mei 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post