Na Mwandishi wetu Mwanza
Wadau wa usafirishaji kwa njia ya maji na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Mwanza na Mikoa ya Jirani wametakiwa kuhakikisha wanatunza mazingira ya ziwa Victoria kwa mustakabali wa uchumi wao na Taifa kwa ujumla
Hayo yamesemwa na Mkufunzi kutoka Taasisi ya DANAOS Shipping Company iliyopo Visiwani Zanzibar Bw. Tumba Said wakati akitoa elimu ya ubaharia na utunzaji wa mazingira ya ziwa Victoria kwa Wasafiri kutoka ndani na nje ya Jiji la Mwanza waliokuwa wakisafiri kutoka jijini humo kuelekea Sengerema kwa kutumia kivuko cha FB MUGENDI ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha vilivyopo katika Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza kuanzia Tarehe 22 mpaka 25 Juni,2023
“ Ziwa Victoria linachukua sehemu kubwa ya Jiji la Mwanza, hii ni fursa kubwa ya kiuchumi na kitalii kwani zaidi ya asilimia 70 ya Mizigo,Mazao , Abiria na bidhaa zinazopatikana hapa na kwenda Mikoa ya Jirani hata nje ya Nchi zinasafirishwa kupitia Ziwa hili, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunayatunza mazingira yake ili liendelee kuwa chanzo kikubwa cha kuboresha uchumi wa wananchi na taifa” amesisitiza Tumba
Mkufunzi Tumba amesema shehena kubwa za mizigo Duniani kote husafirishwa kwa njia ya maji na kwa kuitambua umuhimu wa Mabaharia Shirika la Bahari Duniani(IMO) liliona ni vyema kuitambua siku ya Mabaharia Duniani ambapo kwa mwaka Huu 2023 Kitaifa inafanyika hapa Jijini Mwanza nasi tunayatumia maadhimisho haya kutoa elimu ya ubaharia ,usalama na utunzaji wa mazingira ya usafirishaji kwa njia ya maji
Naye Bi.Fortunata Kakwaya kutoka Jumuiya ya Wanawake waliopo katika Sekta ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) amewataka wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya Jirani kuwapa hamasa watoto wao hasa watoto wa kike waliomaliza kidato cha Nne na Sita kujiunga na chuo cha Mabaharia Tanzania(DMI) ili kuongeza idadi Wanawake Mabaharia wanaoendesha shughuri Mbalimbali za Ubaharia ndani na nje ya nchi
“Wahimizeni mabinti zenu waliomaliza kidato cha NNe na Sita wajiunge na kozi mbalimbali za ubaharia,watembelee kwenye viwanja vya Furahisha wakajiandikishe pale kwani udahili unaendelea” Amesisitiza Bi Fortunata
Maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani mwaka 2023 yenye kauli mbiu “Miaka 50 ya Marpol Uwajibikaji wetu unaendelea” yaliyofunguliwa tarehe 22 Jini, 2023 na Waziri wa Uchumu wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame yatafikia tamati tarehe 25 Juni,2023 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof Makame Mbarawa
Imetolewa na idara ya habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Social Plugin