Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata gunia 482 za bangi iliyokuwa tayari kusafirishwa kwenye masoko na imeteketeza jumla ya hekari 101 za mashamba ya bangi yanayokadiriwa kuwa na bangi mbichi gunia 550 katika eneo la Kisimiri Juu kata ya Uwalu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Ukamataji huo umefanyika Mei 31,2023 kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini.
Akizungumza operesheni hiyo maalumu iliyofanyika mkoani Arusha Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa na hatimaye wakulima na wananchi kwa ujumla wanaoishi katika eneo ya Kisimiri juu na chini wanaachana na kilimo cha bangi na kujikita katika mazao mengine ya biashara badala ya bangi.
Kamishna Lyimo amesema kuwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) katika kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais linatekelezwa, ameelekeza kufanyika kwa utafiti kujua ni mazao gani mbadala yanaweza kulimwa katika maeneo hayo ambayo yamekithiri kwa kilimo cha dawa za kulevya, ili wananchi wa maeneo husika waweze kupewa mbinu mbadala za kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara badala ya kuendelea na kilimo cha bangi.
‘‘Tumewasiliana na Wizara ya Kilimo na Afisa kilimo wa kata ya Uwalu hapa Kisimiri ambaye ameeleza tayari utafiti huo umefanyika",amesema.
Aidha, Kamishna Lyimo amesema, elimu juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya itatolewa kupitia shule za msingi na sekondari.
"Hii inafanyika kufuatia agizo la Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kuitaka Mamlaka kushirikiana na wadau kutoa elimu katika maeno hayo. ambapo tayari maafisa elimu Kata wameanza kutoa elimu kwa wanafunzi, ili baadaye wasijihusishe na kilimo cha bangi na mirungi badala yake wajikite kwenye mazao mengine",ameongeza.
Katika kuhakikisha maagizo ya Waziri Mkuu yanatekelezwa, Afisa kilimo Kata ya Uwelu, Samwel Palangyo, amesema kuwa,utafiti uliofanywa na Wizara ya Kilimo kupitia kituo cha utafiti wa kilimo cha TARI Tengeru, imebaini kuwa yapo mazao yanayostawi katika maeneo hayo kama vile pareto, karoti na viazi mviringo na kuwa mbadala wa zao haramu la bangi ambalo halifai katika jamii.
Ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kwa kutoa ruzuku ya mazao hayo.
Operesheni hii imefanyika ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambapo katika taarifa hiyo alitaja mikoa inayojihusisha na kilimo cha Bangi kwa kiasi kikubwa, Mkoa wa Arusha ukiwa kinara ukifuatiwa na Iringa, Morogoro na Manyara.
Social Plugin