Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAKABIDHI GAWIO KUBWA ZAIDI KUPATA KUTOKEA LA SHILINGI BILIONI 45.8 KWA SERIKALI


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (watatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea gawio la Shilingi bilioni 24.6 kutokana na uwekezaji wa Serikali Kuu kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark kupitia mfuko wa Uwekezaji wa pamoja wa DANIDA kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Hussein Laay (wapili kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kushoto). Wengine pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Dkt. Natu El- Maamry Mwamba (wapili kulia), Prof. Neema Mori Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB (wakwanza kulia), Royal Lyanga, Kamishna Msaidizi wa Mipango na Maendeleo Wizara ya Fedha na Mipango (katikati), na Melckzedeck Mbise, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango.


========= ======== =========


Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Mwigulu Nchemba amepokea gawio kubwa zaidi kupata kutolewa na taasisi ya kifedha la shilingi bilioni 45.8 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.

Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB.

Akizungumza katika hafla hiyo Wazir wa Fedha aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2022 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.

“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2023/2024. “Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dkt. Nchemba.
Aliipongeza Benki ya CRDB kwa kukamilisha mkakati wa muda wa wakati wa 2018/2022 kwa mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita faida ya benki hiyo imekua kwa asilimia 875. “Niwapongeze pia kwa matokeo ya fedha ya robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo Benki yetu hii imepata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 90, mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” alisema Dkt. Nchemba.

Akielezea namna ambavyo Serikali inaridhishwa na umahiri wa Benki ya CRDB katika kufanya biashara kiushindani, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni tanzu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kampuni tanzu ya CRDB Insurance Co. Ltd, pamoja na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imeonyesha kuwa mstari wa mbele katika kuchochea ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU.
Dkt. Nchemba alizitaka taasisi nyengine kuiga mfano wa Benki ya CRDB katika kuleta faida kwa Serikali na Wanahisa kutokana na Uwekezaji. Alizitaka Taasisi na Mashirika yote ambayo Serikali ina hisa kuweka mikakati madhubuti itakayoleta tija, huku akiwataka viongozi ambao taasisi zao zimeendelea kuwa na matokeo mabovu kujitathmini kiutendaji.

Aidha, Dkt. Nchemba aliihakikishia Benki ya CRDB na wadau wengine wa maendeleo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyinginezo ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

Dkt. Nchemba alisema Serikali ina mpango wa kuja na programu kabambe ambayo itasaidia kuboresha sekta binafsi na kupunguza mikopo chechefu nchini. Pia alisisitiza juu ya weledi wa wafanyakazi wa mabenki katika utoaji wa mikopo kwa kuhakikisha fedha zinazokopeshwa zinakwenda kwenye miradi au biashara endelevu.
Naye katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia benki hiyo na kupelekea matokeo mazuri ya kifedha na kukua kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali. Dkt. Natu aliipongeza pia Benki Kuu kwa usimamizi mzuri wa sekta hiyo ambayo imechangia katika utendaji mzuri wa taasisi za kifedha, na uwepo wa huduma bora na nafuu kwa wananchi.
Akikabidhi gawio Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 351.4 baada ya kodi ambayo Benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2022.

“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) mwezi Mei mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 45 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 na hivyo kufanya jumla ya gawio la mwaka huu kufikia shilingi bilioni 117.5,” alisema Dkt. Laay.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kukua kwa thamani ya uwekezaji wa wanahisa wa benki hiyo kutokana na mafanikio ambayo benki hiyo imeyapata katika utekelezaji wa mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa mwaka 2018 – 2022.

Nsekela alisema katika kipindi hicho Benki ya CRDB imepata mafanikio makubwa ya kiutendaji yaliyopelekea benki hiyo kuwa na mchango mkubwa katika kusaidia jitihada za maendeleo nchini. Nsekela alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imelipa jumla ya kodi ya Shilingi trilioni 1.1 kwa serikali.

“Katika kipindi cha miaka mitano pia tumeweza kuongeza ajira zaidi ya 600 nchini, tukitumia zaidi ya Shilingi trilioni 1.3 kulipa mishahara na marupurupu, tumefanya kazi na wazabuni zaidi ya 1,000 na kulipa zaidi Shilingi bilioni 625,” alisema Nsekela huku akibainisha benki hiyo imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 14 katika miradi ya kijamii kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii.

Nsekela alimweleza Dkt. Nchemba kuwa mwaka huu utekelezaji wa mkakati wetu mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano (2023 – 2027) ambao unasisitiza katika “Mageuzi Thabiti”. Kupitia mkakati huo Benki ya CRDB imejipanga kikamilifu katika kuwekeza kwenye ubunifu wa huduma, bidhaa, na programu zitakazosaidia kuboresha maisha ya watu na uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.

Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, pamoja na halmashauri Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 15.














Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com