DCEA YAKAMATA DAWA ZA KULEVYA DAR, PWANI, ARUSHA NA KILIMANJARO.....RAIA WA KIGENI WATUMIA MBINU YA MAPENZI


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo

TAARIFA KWA UMMA UKAMATAJI WA DAWA ZA KULEVYA KATIKA MIKOA YA DAR ES SALAAM, PWANI, KILIMANJARO NA ARUSHA 

Dar es Salaam, 19 Juni, 2023: Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5, bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5, methamphetamine gramu 531.43, heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza ekari 1,093 za mashamba ya bangi.

 Aidha, kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) Mamlaka imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya. 

Ukamataji huo uliofanyika kuanzia tarehe 25 Machi, 2023 hadi tarehe 19 Juni, 2023 unahusisha watuhumiwa 109 wakiwemo raia watatu wa kigeni. 

Baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani na wengine wanatarajiwa kufikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika. 

Kutokana na udhibiti kuwa mkubwa, wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kubuni mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya ili kukwepa kukamatwa. 

Mamlaka imebaini mbinu hizo na kuchukua hatua. Mbinu mojawapo inayotumika ni raia wa kigeni  kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanawake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa za kulevya kwenye makazi ya wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na wanakoishi wapenzi wao. 

Hali hii husababisha wanawake wa kitanzania kuingia kwenye matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku wanaume wakiwakana wanawake hao. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imejipanga kikamilifu kupambana na biashara ya dawa za kulevya. 

Hivyo, wote wanaojihusisha au wenye mpango wa kujihusisha na biashara hiyo, waache mara moja au wajisalimishe wenyewe kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria. Pia, wananchi wanapaswa kuwa makini na mizigo wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini. 

Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakitumiwa na wapenzi wao hasa raia wa kigeni kusafirisha na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za kulevya na hivyo hujikuta matatani. 

Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani.

 Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii. Kutokana na kuwepo madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya, ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hili. 

Aidha, katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanatokomea nchini, Mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii. 

Ili kupanua wigo wa utoaji elimu, Mamlaka imeingia makubaliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutumia klabu zao zilizokwisha anzishwa kwenye 3 shule na vyuo kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya.

 Hivyo, elimu ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya itatolewa kupitia klabu hizo. Vilevile, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawataarifu watu wote kuwa, tarehe 26 Juni kila mwaka, Tanzania huungana na Mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha Umma kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

 Maadhimisho haya kwa mwaka huu kitaifa, yatafanyika tarehe 23 Juni, hadi tarehe 25 Juni, 2023 jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Maadhimisho haya yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti zinazofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wake katika udhibiti wa dawa za kulevya na utoaji elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya. 

Mgeni rasmi siku ya kilele tarehe 25 Juni, 2023 ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Tuzingatie Utu na Kuboresha Huduma za Kinga na Tiba”. 

Wananchi wote hususani wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani mnakaribishwa kushiriki katika maadhimisho hayo.

 Imetolewa na, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post