Jengo la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Shinyanga limeteketea kwa moto na kuunguza maduka saba yaliyokuwa kwenye jengo hilo pamoja na mali zilizokuwa ndani huku maduka sita yakinusurika.
Katika tukio hilo, mali za Wafanyabiashara ambazo thamani yake bado haijajulikana, zimeteketea kwa moto ulitokea usiku wa kuamkia leo Juni 6, 2023 katika jengo hilo la maduka linalomilikiwa na Umoja wa Wanawake Tanzania UWT mkoa wa Shinyanga, maarufu kama JJ, lilipo mkabala na ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoa wa Shinyanga.
Moto huo ambao unadaiwa kuanza kuwaka majira ya saa tisa usiku katika jengo hilo ambalo lina jumla ya maduka 13 na kuunguza maduka saba na mali zote zilizokuwa ndani.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, moto huo umeanza majira ya saa nane usiku na kusababisha vyumba saba vya maduka kuungua huku sita vikiokolewa.
Wakizungumza kwa masikitiko makubwa, baadhi ya wafanyabishara waliopoteza mali zao, wamesema walipigiwa simu usiku na mlinzi wakijulishwa kuhusu maduka yao kuteketea kwa moto, ambapo walitoa taarifa kwa Jeshi la zima moto na kufika kujaribu kuuzima moto huo, baada ya magari ya Jeshi hilo kuchelewa kufika katika eneo la tukio.
Baadhi ya Wafanyabiashara ambao Maduka yao hayakuteketea Moto, wamelipongeza Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kwa kufika kwa wakati eneo la tukio na kufanikiwa kuzuia moto huo usiteketeze maduka yote.
Akizungumzia tukio hilo Katibu wa UWT mkoa wa Shinyanga Bi. Asha Kitandala, amesema tukio hilo limewarudhisha nyuma Wafanyabishara waliokuwa wakifanyia biashara katika jengo hilo na kwamba, UWT pia walikuwa wakilitegemea kwa mapato.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa,umetokana na hitilafu ya umeme.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga Mrakibu Martin Nyambala, amesema Jeshi hilo lilipata taarifa ya Moto huo majira ya saa 9 usiku, na walipofika eneo la tukio walifanikiwa kuzima maduka Sita lakini saba yaliteketea moto.
“Chanzo cha Moto huu bado kinachunguzwa, lakini tunatoa wito kwa wafanyabiashara wawe na vizimia moto kwenye maduka yao pamoja na kutoa taarifa mapema hasa kwa walinzi wanapoona matukio ya moto wasipige simu kwanza kwa mabosi wao bali wapige kwa Jeshi la Zimamoto kwa namba 114,”amesema Nyambala.
Social Plugin