Watu 15 wa familia moja wameaga dunia nchini Namibia baada ya kunywa uji ulioharibika.
Hili ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi nchini humo ya maafa yanayotokana na chakula kibovu.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa familia hiyo ambayo ilikuwa imepigwa na njaa kupitiliza ilikunywa uji huo kutoka kwa mabaki ya nafaka ya kutengeneza pombe.
Polisi wanasema kuwa wanatoka katika familia ya watu 21 katika kijiji kimoja eneo la Kavango Mashariki linalopatikana Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi Kauna Shikwambi, watu hao 15 waliofariki walianza kuugua baada ya kula chajio mnamo Jumamosi na kukimbizwa hospitalini.
"Kufikia sasa hii ndio idadi kubwa zaidi ya vifo kuwa kutokea kwa sababu ya kula chakula chenye sumu au kilichoharibika," Shikwambi amenukuliwa na AFP.
Shikwambi anasema kuwa Jumatano, watu 15 walikuwa wamefariki na kuongeza kuwa uchunguzi umeanza huku majibu ya upasuaji na vipimo vya maabara vikisubiriwa.
Social Plugin