Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGODI WA BARRICK BULYANHULU WAJENGA SHULE MPYA YA BWENI YA SEKONDARI YA WASICHANA YA VIPAJI MAALUM


MGODI WA BARRICK BULYANHULU WAJENGA SHULE MPYA YA SEKONDARI YA WASICHANA

Na Marco Maduhu,KAHAMA

MGODI wa uchimbaji Madini ya Dhahabu Barrick Bulyanhulu  uliopo Halmashauri ya wilaya ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, umejenga Shule mpya ya Sekondari ya Bweni ya Wasichana ya Vipaji Maalum katika kijiji cha Buswangili Kata ya Bulyanhulu.

Kaimu Meneja Mahusiano ya Jamii Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Zuwena Senkondo, amebainisha hayo jana wakati Timu ya Waandishi wa Habari kutoka Mkoani Shinyanga ilipokuwa ikifanya ziara ya kuangalia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa ndani ya jamii na Mgodi huo.

Amesema Mgodi huo katika uwajibikaji kwa jamii umetekelezwa miradi mingi ya maendeleo kwa jamii,na mwaka huu wapo kwenye ukamilishaji wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya wasichana ya vipaji maalum ambayo itaanza kutoa elimu mwakani.

“Shule hii mpya ya Sekondari ya Wasichana ya Bweni ambayo ipo katika kijiji cha Buswangili Kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala itakuwa ya vipaji maalum, na itatoa elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi Nne, na itagharimu kiasi cha Sh,milioni 800,”amesema Senkondo.

Naye Msimamizi wa ujenzi wa Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata Bulyanhulu James Mukasa, amesema shule hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa kike katika kutimiza ndoto zao, na kuacha kurubuniwa na wanaume na kuingia kwenye mapenzi na kupata ujauzito.

Amesema wanafunzi ambao wanasoma katika Shule Mama ya Kata Bulyanhulu, baadhi wanasoma umbali mrefu zaidi ya Kilomita 14 hadi 15, kwamba hivyo ni virahisi wanafunzi wa kike kuingia kwenye mitego ya wanaume na kuangukia katika mapenzi na hatimaye kupata ujauzito na kuacha masomo.

Aidha, amesema ujenzi wa shule hiyo umeshakamilika kwa asilimia 96 na tayari kuna Viti na Meza 320 ambavyo vitatumiwa na wanafunzi 320 watakaoanza kidato cha kwanza mwakani, na pia itapunguza msongamano wa wanafunzi katika shule Mama ambao wapo 2,700 na kusoma katika mazingira Rafiki na kuelewa vizuri masomo.

Mtendaji wa Kijiji cha Buswangili Asifiwe Ally, ameupongeza Mgodi huo wa Bulyanhulu kwa ujenzi wa Shule hiyo mpya ya Sekondari ya Wasichana, na kueleza kuwa ilikuwa ni shauku kubwa ya wazazi kuona watoto wao wanasoma shule karibu na katika mazingira salama ya kuishi bweni.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Bulyanhulu James Mukasa, akielezea hatua za ujenzi wa shule hiyo mpya ya Sekondari ya Wasichana na faida yake katika kukomboa mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata Bulyanhulu James Mukasa, akionyesha Viti na Meza 320 ambavyo vitatumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani katika shule mpya ya Secondari ya Wasichana (Bulyanhulu Girls Sekondari School).
Muonekano wa vyumba vya Madarasa katika shule hiyo mpya ya Sekondari ya Wasichana, Bulyanhulu Girls Sekondary School.
Muonekano wa vyumba vya Madarasa katika shule hiyo mpya ya Sekondari ya Wasichana, Bulyanhulu Girls Sekondary School.
Muonekano wa Maabara za Sayansi katika Shule hiyo Mpya ya Wasichana, Bulyanhulu Girls Sekondary School.
Muonekano wa Hosteli ya Wasichana katika Shule hiyo mpya ya Bulyanhulu Sekodary School.
Mafundi wakiendelea na ujenzi ili kukamilisha ujenzi wa Shule hiyo Mpya ya Sekondari ya Wasichana, ambayo mwakani itaanza kutoa elimu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com