Kama ulidhani kutokukamilika kwa mradi wa mwendokasi awamu ya pili kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu kunawakera wakazi wanaohangaika na usafiri kila linapokucha au kukuchwa unajidanganya. Ipo adha nyingine ya vituo vyake kugeuzwa madanguro, walalamikiwa wakubwa wakiwa baadhi ya askari polisi wanaodaiwa ‘kutengeneza fedha’ kupitia biashara hiyo ya ngono.
“Naogopa kusema, nikikuambia tutakuwa hatuachiwi tena. Au lengo lako tulale ndani? (rumande),”anauliza Grace.
“Pale inategemea, magari ya doria yanapita kuanzia saa nne usiku hadi saa tano usiku hayo hayakamati watu, lakini yapo matatu yanapita kuanzia saa sita hadi saa saba usiku hayo ndiyo yanakuwa na askari wenye sare na wasio na sare (anawaita sungusungu). Hao ndio hukamata,”anasema.
Grace anasema askari wasio na sare huwakamata na kuwapandisha katika gari kisha kuwachukulia fedha na kisha kuwaacha waendelee na biashara yao.