Afisa wa polisi anauguza majeraha kwenye sehemu zake za siri baada ya kuanguka kutoka kwenye mlingoti wa bendera akiishusha bendera ya taifa.
Kulingana na taarifa ya polisi, tukio hilo lilitokea baada ya afisa huyo wa katika kituo cha polisi cha Shelly Beach, Mombasa nchini Kenya kupanda mlingoti wa bendera ili kuishusha bendera baada ya kamba kukatika na kuacha bendera ikining'inia juu ya mlingoti huo.
"Mara tu alipoanza kuishusha bendera, kamba ilikatika na kuacha bendera ikining'inia juu ya mlingoti. Kwa hiyo, akaamua kupanda mlingoti na kuitoa. Hata hivyo, alipokuwa akishuka, alishtuka na kuanguka kutoka kwenye mlingoti huku akiwa na bendera mkononi," ilisoma sehemu ya ripoti ya polisi.
"Vifaa vya chuma vinavyoshikilia kamba chini ya mti vilichoma sehemu zake za siri na akajeruhiwa vibaya," ripoti iliongeza.
Ripoti hiyo pia iliongeza kuwa maafisa wa zamu walitembelea eneo la tukio na kumpata afisa huyo akiwa na majeraha na kumbikiza katika hospitali ya Diani kwa matibabu.
Social Plugin