Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. NDALICHAKO : TUTAHAKIKISHA WAONGOZA WATALII WANAKUWA NA UJUZI STAHIKI






Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako,akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa Wafanyakazi waongoza watalii 600 iliyofanyika jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunga mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa Wafanyakazi waongoza watalii 600 iliyofanyika jijini Arusha.



Na Mwandishi Wetu, Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amesema serikali imedhamiria kuhakikisha wafanyakazi waongoza watalii wanakuwa na ujuzi stahiki ili kuunga juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya utalii nchini.

Prof. Ndalichako ameyasema hayo Juni 17, 2023 kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa Wafanyakazi waongoza watalii 600 iliyofanyika jijini Arusha.

Amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi iliyopo chini ya Ofisi yake ili kuunga mkono jitihada anazofanya Rais kupitia The Royal Tour filamu ambayo inatangaza vivutio vya utalii inayolenga kuiimarisha na kuikuza sekta hiyo.

Amebainisha kuwa kabla ya kutoa mafunzo Wizara ilitembelea hoteli kubwa 35 pamoja na kufanya majadiliano na Chama cha Waongoza Watalii Tanzania na kubaini changamoto zinazowakabili waongoza watalii nchini ikiwemo upungufu wa ujuzi.

"Tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Utalii ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata ujuzi na weledi wa kuhudumia watalii kwa kuwapa hamasa ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini" amesema

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Saidi Mabie, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango amesema programu imetolewa kwa kuzingatia maeneo manne ambayo ni mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya uzoefu wa Kazi kwa wanaohitimu elimu ya juu, mafunzo ya urasimishaji ujuzi usiopatikana katika mfumo rasimi na mafunzo ya kukuza ujuzi Kwa sekta za Umma na binafsi.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi Tanzania (TANAPA) Batiho Herman amesema miundombinu zote katika hifadhi 22 zimeboreshwa ili kuwavutia watalii wa nje na ndani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com