Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua Baraza jipya la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na kulitaka Baraza hilo pamoja na mambo mengine kuhakikisha linajenga mifumo ambayo itasaidia kujua aina ya nguvu kazi inayohitajika na waajiri ili iweze kuzalishwa chuoni hapo.
Akizungumza mara baada ya kuzindua baraza hilo Waziri Mkenda amesema mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha tunaongeza kasi ya uwekezaji hivyo ni vizuri kujenga mifumo hiyo na kuimarisha uhusiano na wanaohitaji taaluma za wahitimu kutoka DIT
“Kuna viwanda vipya vingi vinajengwa sasa hivi hasa Mkoa wa Pwani na nchi nzima, mwelekeo wa Serikali ni kuongeza uwekezaji sasa viwanda ambavyo vinajengwa ningeomba Baraza litusaidie kujenga mfumo ambao utatusaidia kujua vinahitaji nguvu kazi ya namna gani,”amesema Prof. Mkenda.
Amesema moja ya changamoto iliyopo sasa ni wawekezaji kutopata nguvu kazi yenye ujuzi hivyo DIT fanyie kazi hilo na kama ikionekana hakuna wataalamu wa kutoa mafunzo hayo fuateni taratibu kupata wataalamu kutoka kwenye vyuo vya nje kuja kufundisha.
“Nendeni TIC angalieni nani wanajenga viwanda na wanajenga wapi aina gani ya viwanda vinajengwa wafuateni wahusika muwahoji baada ya kukamilisha wanahitaji nguvu kazi ya aina gani ili mtengeneze program hata kama ni za muda mfupi lengo ni kuwaandaa watanzania kwa ajili ya ajira ya aina hiyo,”amesema Prof. Mkenda.
Akizungumzia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia Chuoni hapo Waziri Mkenda amelitaka Baraza hilo kuhakikisha linaimarisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika kakarana za chuo hicho.
“Miundombinu ni muhimu sana na itaendelea kuwa muhimu lakini tukienda kwenye miundombinu tunachukua muda sana, wanafunzi wakishaanza masomo ni kama mkono wa saa unatembea kwa hiyo hatutaki wakae hapa halafu vifaa vinachelewa. Ningependa mkaangalie huko duniani teknolojia kwa sasa ikoje akitolea mfano China na India ili karakana zetu ziwe na vifaa vya kutosha na sahihi kulingana programu za mafunzo na idadi ya wanafunzi,”ameongeza Prof Mkenda
Pia amelitaka Baraza kuhakikisha bunifu zinazozalishwa na DIT zinaendelezwa na kubiasharishwa ili Chuo kiendelee kuzalisha bunifu zaidi na ziwe na tija huku akiwataka kendelea kuimarisha mahusiano ya kimataifa ili wanafunzi wapate fursa za kusoma vyuo vya nje na kurejea lakini pia wahadhiri kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza jipya la DIT Dkt. Richard Masika amesema baraza hilo ambalo ni la nane kwa Chuo hicho lina hamasa ya kufanya kazi na tayari limeshaanza kazi kwa kufanya ziara Kampasi ya DIT mwanza kuona maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayofadhiliwa na Mradi wa EASTRIP.
Social Plugin