Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Baraza la wazee, viongozi wa dini na Machifu Mkoani Shinyanga wameuunga mkono makubaliano ya uwekezaji kwenye bandari ya Dar es salaam kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni yake ya DP World wenye lengo la kuanzisha ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini.
Tamko hilo limetolewa leo Juni 16,2023 kwenye kikao na uongozi wa mkoa huo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni Siku chache baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha azimio la kuridhia Mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania.
Akisoma tamko hilo lililopitishwa kwa makubaliano ya watu wote na kusomwa na Chief wa Kizumbi Chief. Charles Njange amesema wamekubaliana na kuunga mkono makubaliano ya uwekezaji uliofanywa baina ya nchi hizo mbili na kulaani wale wanaopotosha jamii juu ya makubaliano hayo kwa uchochezi wa maneno yasiyokuwa na tija na staha.
“Sisi wazee, viongozi wa dni na machifu wa Mkoa wa Shinyanga tunakubali na kuunga mkono makubaliano haya yaliyofanywa na serikali yetu ya awamu ya sita, kwani haya ni mahusiano mazuri ya kiuchumi baina ya nchi hizi mbili, lengo la serikali yetu ni jema kwani serikali inapambana kutuletea maendeleo katika nchi yetu”, amesema Chief. Charles Njange.
"Wazee tunalaani kitendo cha baadhi ya watu wachache wanaotaka kumpaka matoke Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa kusema ameuza bandari kwa falme za kiarabu,inatupasa kutumia busara ya kawaida na kuwakataza wengine wanaopotosha, tuungane na viongozi wetu kuleta maendeleo katika nchi yetu, tunabariki na kuunga mkono jitihada hizo", ameongeza Chifu Charles Njange.
Awali akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ameeleza manufaa yatakayopatikana ndani ya mkoa kutokana na makubaliano ya uwekezaji wa bandari ya Dar es salaam ambapo amesema kuwa ndani ya mkoa wa Shinyanga kuna bandari kavu mbili zitakazotoa fursa za ajira kwa vijana mpaka sasa mkoa wa Shinyanga umepokea Shilingi Bilioni 612.3 kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.
Nao baadhi ya wazee walioudhuria kikao hicho akiwemo Fransisca Ngokolo na Mohamed Mkambala wamesema kuwa maendeleo ya nchi yanaletwa na juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Shinyanga ni moja ya Mikoa inayonufaika na fedha za serikali kwenye miradi mbalimbali hivyo wataendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita.
Chief wa Kizumbi Chief. Charles Njange akisoma tamko wakati wa kikao.
Baadhi ya washiriki walioudhuria kikao hicho.
Baadhi ya washiriki walioudhuria kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude wakati wa Kikao.
Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Habibu akichangia wakati wa kikao hicho.
Social Plugin