Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIT KUZALISHA WATAALAM WENGI KUPITIA KITUO CHA UMAHIRI CHA TEHAMA


***************

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inatarajia kutoa wataalam wa kutosha katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ngozi na nishati jadidifu vitakavyochochea ukuaji wa uchumi wa jamii na Taifa mara baada ya kukamilika kwa vituo vinne vya umahiri vinavyojengwa kwenye Kampasi Kuu na Mwanza.

Tanzania inatekeleza Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP) uliofadhiliwa na Benki ya Dunia unaojenga Kituo cha Umahiri wa Tehama cha Kikanda (RAFIC), Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa Teknolojia ya Ngozi (CELPAT), Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu Arusha na Kituo cha Umahiri cha Usafirishaji NIT.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati wa ziara iliyolenga kutembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha RAFIC kilichopo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi kuu Dar es Salaam ili kuona hatua iliyofikiwa.

"kituo hicho kikikamilika tunatarajia kupata wataalamu wa kutosha kabisa katika masuala ya Tehama ambao sasa wataendana na mapinduzi ya viwanda" amesema Prof. Mdoe.

Ameeleza kuwa, lengo kubwa la kuanzishwa kwa vituo hivyo ni kuweza kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwa kila kimoja kitakuwa na mchango chanya katika kutatua changamoto za jamii na pia kuchochea maendeleo ya taifa.

Amesema "maendeleo ya ujenzi huu wa Kituo hiki mahiri cha Tehama unaenda vizuri na tunatarajia utakamilika kabla ya muda uliopangwa ili wanafunzi waweze kupata fursa ya kupata ujuzi katika Tehama utakaochochea ukuaji wa uchumi hali kadhalika kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda".

Aliongeza kuwa; "Mradi huu wa EASTRIP umeanza mwaka 2021 na tunatarajia utakamilika mwaka mwezi disemba mwaka 2024 huku akielezea majukumu makubwa ya mradi ikiwa ni pamoja na kusomesha wakufunzi, kuboresha mitaala na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo na viwanda ili wanafunzi watakaomaliza wapate ujuzi unaotakiwa viwandani," alisema Profesa Mdoe.

Ameongeza kuwa matarajio ni kwamba kituo cha Tehama kitakamilika kabla ya muda uliopangwa na wanufaika 4,250 watazalishwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa mradi huo, Dk John Msumba amesema kuwa kituo hicho kikikamilika kitasaidia Watanzania katika kuongezwa uelewa wa masuala ya Tehama .

Dkt. Msumba ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Tanzu ya DIT, amesema Tanzania haitabaki nyuma kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanahitaji wataalamu mahiri katika matumizi ya Teknolojia kwa kuwa kupitia kituo hiki idadi kubwa ya watu watafikiwa na hii itapanua wigo wa kuwa wataalam hawa kwa wingi.

Afafanua kuwa Taasisi ya DIT imeaminiwa katika kusaidia vijana wapate elimu na ujuzi katika Tehama lengo likiwa ni kukuza uchumi na maendeleo ya nchi na ya mtu mmoja moja kwa ujumla.

Katika mradi huu, chuo kimepewa Sh bilioni 74 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha RAFIC ambao mpaka sasa umefikia asilimia sita ya utekelezaji na Kituo cha CELPAT ambao umefikia asilimia 20.

Pia serikali ilitoa Sh bilioni 37 kwa Chuo cha Ufundi Arusha ambacho kinajenga Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu ambacho kitazalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji, mionzi ya jua, upepo, tungamo taka pamoja na kujenga mitambo itakayowezesha kuzalisha umeme wa nguvu za maji wa megawati 1.65.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com