Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Watoto wawili wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia baada ya kufukiwa/kupondwa na mawe wakati wakichimba mchanga katika eneo la Marahara kijiji cha magata kata ya Karutanga wilayani Muleba mkoani Kagera .
Diwani wa Kata ya Magata Karutanga Alhaji Yakubu Mahamudu amesema kuwa watoto hao walipotea Juni 26 ,2023 na walitafutwa maeneo yote hawakuweza kupatikana na June 27 watoto hao walipatikana wakiwa tayari wamefariki dunia baada ya kufukiwa na mawe wakati wakichimba mchanga.
Alhaji Yakubu amewataja watoto hao kuwa ni Samsoni Eliud mwenye umri wa miaka 13 na Emmanuel Eliud mwenye umri wa miaka 10 ambapo wote walikuwa wanafunzi wa shule ya Msingi Magata na kuongeza kuwa watoto hao waliterekezwa na baba yao mzazi na kubaki na mama yao pekee .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amefika katika eneo hilo ambapo amepiga marufuku na kuzuia mtu yoyote yule kufanya shughuli za uchimbaji wa mchanga kwani eneo hilo sio salama na kuagiza kukaguliwa maeneo yote ya uchimbaji wa mchanga katika wilaya hiyo ili kudhibiti maafa yasiendelee kutokea.
Nao baadhi ya wananchi ambao ni Ashimu Salimu na Godfrey Joel wamesikitishwa na tukio hilo na kuwahimiza wazazi kuendelea kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuwahimiza wanaume kutowatelekeza watoto.
Social Plugin