Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,amechangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na kutoa ombi kwenye maeneo matatu ikiwemo kwa serikali kuja na mpango mahsusi wa kuendeleza mradi wa umeme wa upepo Mkoani Singida ambao utekelezaji wake umekwama.
Akichangia Mei 31,Bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema mradi huo ukifanya kazi utawezesha kuongeza umeme katika Gridi ya Taifa.
Amesema juzi amemuona Waziri wa Nishati Januari Makamba akisaini mkataba wa umeme wa jua pale Kishapu Mkoani Shinyanga jambo ambalo ni zuri na la kupongezwa.
“Mh Waziri hili ni jambo zuri sana,lakini tumekuwa na kilio cha muda mrefu cha umeme wa upepo,na umeme huu tumezungumzia Makambako,tumezungumzia Singida,hivi ninavyoongea kuna watu wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye mradi huu lakini mpaka sasa bado hatujaona dalili yoyote ya kuanza umeme huu ,umeme huu ni wa uhakika,hautaangalia mabadiliko ya tabia nchi,
“Nikuombe sana unapokuja utuambie mipango mahsusi ya wizara ili kuunasua mradi huu,kumekuwa na siasa nyingi naomba hizo siasa tuziondoe tuhakikishe mradi ule wa Singida uanze mapema ili tuweze kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa wakati tunasubiri vyanzo vingine,”amesema.
SUALA LA WATUMISHI WA TANESCO.
Mtaturu amesema ili Shirika la Umeme Nchini(TANESCO),liweze kufanya kazi vizuri ni lazima kuwe na mitambo,mashine,teknolojia,fedha za kuwekeza na kuwa na rasilimali watu wenye furaha.
“Ukishakuwa na rasilimali watu wenye furaha,motisha na wenye kupewa msaada muda wote utafanya kiwanda ambacho ni TANESCO kifanye kazi vizuri ,kama ambavyo nimemsikia Mh Mkundi amesema asubuhi hapa kwamba kumekuwa na manung’uniko kidogo upande wa wafanyakazi wa Shirika hili,kumekuwa na dalili huwenda Shirika likapunguza wafanyakazi,
“Sasa Mh Waziri leo hii unao wateja Milioni 4 nchi nzima lakini unao wafanyakazi 9900,wastani wa mfanyakazi mmoja anahudumia wateja 424,maana yake ni kwamba kuna mfanyakazi mmoja anahudumia wateja wengi sana hivyo huwezi kutegemea tija pale,sasa unapotaka kwenda kupunguza wafanyakazi maana yake unaenda kupunguza uwezo wa kuwahudumia wateja,”amefafanua.
Amesema hivi sasa wanaendelea kutekeleza miradi ya umeme vitongojini maana yake kwamba wanaenda kuongeza idadi ya wateja,sasa unapofikiria kupunguza wafanyakazi usitegemee kuwa na huduma zenye tija.
“Tumeendelea kupata taarifa kwamba mnapita kwenye Mikoa kuwaambia wafanyakazi kuwa kuna mpango wa kuwapunguza,mfano Mkoa wa Ilala wa kitanesco una wafanyakazi 288 sasa unasema utabakiza wafanyakazi 86 watahudumia vipi,Mkoa wa Dodoma kadhalika una wafanyakazi 162 unategemea wabaki 86 watahudumiaje wateja wa mkoa huo,
“Hapa maana yake ni kwamba unaenda kuanguka,unaenda kufeli ,nikuombe sana Mh Waziri najua hili huna taarifa nalo ila kumekuwa na fukuto la ndani kwa ndani linaendelea kwenye menejimenti,lifanyie kazi waite vyama vya wafanyakazi mzungumze hili muwafanye wafanyakazi hawa waendelee kufanya kazi ambayo tunaitegemea,”amesisitiza.
Mwisho
Social Plugin