Na Edmund Salaho - Kimotorok Simanjiro
Mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro Mkoani Manyara uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 umefikia tamati baada ya kuwekwa mipaka mipya ya Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo wananchi wa Kijiji hicho wamepatiwa eneo la kilomita za mraba 17.77 sawa na ekari 4392.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Afisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Michael Gwandu, aliwataka wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro ambayo serikali inalazimika kutumia gharama kubwa kuitatua.
Afisa Wanyamapori Mkuu ambae pia anashughulikia kitengo cha utatuzi wa migogoro ya maeneo yaliyohifadhiwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Pellage Fransis Kauzeni, alisema zoezi hilo linatekelezwa kufuatia ushauri wa Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta iliyoundwa na serikali ili kukusanya maoni kuhusu migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi.
Bw. Pellage aliongeza kuwa eneo hilo litasaidia wananchi hao ambao walishaanza kulitumia kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo kilimo, malisho na makazi.
Na kuongeza kuwa wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo linazingatia kutokuingilia mfumo wa ikolojia na kubainisha kuwa mojawapo ya maagizo ya Baraza la Mawaziri baada ya uamuzi wake ni kuwekwa alama za kudumu zinazoonekana ili iwe rahisi kila mmoja kuona mpaka wake.
Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - Beatrice Kessy, amesema kamati hiyo ilishauri kilomita za mraba 17.77 ambazo ni sawa na hekari 4,392 zimegwe katika eneo la hifadhi na kurejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Aidha, Kamishna Kessy alisema eneo linalowekwa mpaka huo lina urefu wa kilomita 10 ambalo wanatarajia kuweka vigingi 30 na hadi sasa wameweka vigingi 22 na kuwa zoezi hilo lililoanza Juni 12,2023 litakamilika kabla ya Juni 30.
Pia, aliongeza mgogoro huo wa zaidi ya miaka 20 ulisababisha shughuli za uhifadhi, doria, uwekezaji na shughuli za wananchi kushindwa kutekelezwa, hivyo wanaamini baada ya kuisha kwa mgogoro mahusiano baina ya hifadhi na wanakijiji yataboreka zaidi ikiwa ni pamoja na shughuli za uhifadhi na utalii zitaendelea.
"Mgogoro huu umechelewesha maendeleo ya wananchi na shughuli za uhifadhi na utalii katika upande huu wa Kusini mwa Hifadhi ya Taifa Tarangire, kwa sasa shughuli za utalii zitafanyika kwa sababu hata ukimpa mwekezaji kuwekeza itanufaisha jamii na kusaidia kuendeleza uchumi wa kijiji na kuchangia kwenye pato la taifa,kuliko ilivyokuwa awali ambapo huwezi hata kuendeleza shughuli za utalii mfano kuanzia walking safari," alisema Kamishna Kessy.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kimotorok,Elias Pamelo, amesema wanatarajia baada ya mgogoro kuisha ujirani baina yao na hifadhi hiyo utaimarika na kuomba serikali kuangalia namna ya kusaidia maeneo machache ambayo bado yako nje ya kijiji hicho kurudishwa kwao.
"Mgogoro huu na sisi kama wananchi tunatamani uishe kwa sababu ni wa muda mrefu ila tunaomba serikali kwenye mapungufu ni kidogo hivyo tutakapopata nafasi tena licha ya kuwa tumepewa eneo kubwa ambalo awali lilikuwa la hifadhi ila kuna eneo ambalo limeonekana ni la hifadhi na tulikuwa tunatumia kwa ajili ya malisho,makazi na mashamba tungeomba hilo tuongezewe,"amesema
Naye, mzee wa mila la kabila la kimasai Laigwanan,Loserian Siria, alishukuru serikali kwa utatuzi wa mgogoro huo na kuomba kuangalia namna serikali inaweza kuongeza eneo kwa ajili ya kijiji hicho ambalo limeonekana kuwa ndani ya hifadhi huku kukiwa na maboma kadhaa ndani yake.