MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Wilaya ya Manyoni na Ikungi zilizopo Mkoani Singida ili kuondoa adha ya kukatika mara kwa mara katika maeneo hayo.
Mbunge Mtaturu ametoa ombi hilo Mei 31,2023,wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2023/2023.
“Mh Waziri ninajua mna miradi ya gridi imara na inafanya kazi vizuri,niombe sana tuangalie maeneo yanayokatika umeme mara kwa mara kama Manyoni na Ikungi hali inayosababisha uwepo wa malalamiko mengi,mi naamini tukiimarisha umeme tutafanya uchumi kwenda mbele na tutafanya watu wafanye kazi zao vizuri kwa uhakika na wafurahie kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu Mh Samia Suluhu Hassan,”amebainisha.
OMBI LA UMEME KWENYE VITONGOJI.
Amempongeza Waziri Makamba na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya inayowapa heshima kama Taifa.
“Tunaona tunaelekea vizuri kwenye miradi ya REA,na kwenye hotuba ya Waziri tumeambiwa asilimia karibu 82 sasa inapata umeme hili ni jambo zuri,tukiangalia tumebakiwa na asilimia 18,na bado tunaona miradi mingi inaendelea kutekelezwa,mi nilitaka kushauri tu Jimbo langu la Singida Mashariki nilikuwa na ugomvi mkubwa na Wizara yako,nilikuwa na tatizo la Tarafa nzima ya Mungaa ilikuwa haina umeme hata kijiji kimoja lakini katika vijiji vile 26 leo ninavyoongea vijiji vyote vimewekewa nguzo na asilimia 40 vimeshawashwa umeme,
Amesema hiyo maana yake ni kwamba na wao wameonja keki ya Taifa kwenye upande wa umeme na kwa namna anavyoona ikifika Disemba mwaka huu kama wakandarasi wataenda anaamini vijiji vyote vilivyobakia vitapata umeme.
“Nasema hivi kwa sababu kuna Tarafa ya Ikungi ambayo ilianza kupata umeme ilikuwa na tatizo la baadhi ya vijiji kama Ng’ongosoro ,Matongo na Mbwanjiki lakini hivi tunavyoongea hatuna ugomvi na wewe umeme unaenda kuwaka,
“Sasa hoja yangu ambayo tunaisema wote, tunaenda kumaliza vijiji lakini tuna tatizo la vitongoji ,nikuombe sana vitongojini ndiko waliko wananchi ,nikuombe sana hivyo unasema angalau vitongoji 15 Mh Waziri havitoshi, tutakuwa na kelele kubwa sana ,nikuombe sana kama utaweza unapokuja kuhitimisha utueleze namna ambavyo utakuwa na mipango ya muda mfupi ya kuongeza angalau tuvifikie vitongoji vingi kwani huko ndipo walipo watu ndipo zilizopo kaya,”amesema.
Amesema Kilomita mbili ambazo walikuwa wanapata hazitoshi kwenda popote na anaamini zitagusa maeneo machache sana.
“Sasa Mh Waziri kwak uwa umeme kila mmoja anapouona anatamani na kwake upatikane,ninajua wewe ni msikivu ,ni kijana mwenye nguvu na Mh Rais amekuamini kusimamia hii sekta,naomba wananchi wa kule kijijini nao waweze kupata umeme kama ambavyo wengine wanapata,”ameomba.
Social Plugin