Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog, DODOMA.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amewataka wadau wa michezo nchini kutumia michezo kutangaza vituo vya Utalii vilivyopo Jijini hapa ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza Utalii wa ndani.
Shekimweri amesema hayo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutambulisha rasmi maandalizi ya Mbio za Mtembezi zitakazofanyika Julai 1,2023 Jijini Dodoma na kuandaliwa na Mtembezi Adventure Kwa kushirikiana na Ofisi yake kwa lengo la kuhamasisha Utalii wa Ndani.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuvitangaza vivutio vingi vya kihistoria vilivyopo mkoani hapa huku vingi vikiwa vimebeba historia ya Mkoa wa Dodoma
na kutolea mfano asili ya neno Dodoma ambalo Tembo alididimia na kuzama moja kwa moja na kupelekea wenyeji na wakazi wa eneo hilo lililopo Kata ya Kikuyu kukiita kitendo hicho Idodomya yaani imedidimia na kupelekea Mkoa huo kuitwa Dodoma hadi leo.
"Dodoma tuna michoro ya mpango,mapori ya swagaswaga na wanyama wapo,tunataka kupitia mbio hizi za Mtembezi watu wajue Dodoma ni sehemu ya Utalii Kwa kuwa tuna vivutio vya kutosha, watanzania wanatakiwa kuipenda asili yao na kuijua kwa kina hivyo ni wajibu wetu kupitia michezo tuwe vinara wa kutunza asili ya utanzania,"amesema.
Naye Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Jeshi la uhifadhi Ofisi ya TANAPA Dodoma Dkt.Noelia Myonga ameielezea Tasisi ya mtembezi Adventures, kuwa ni mfano kwa kuwa kinara kuhamasisha Utalii kwa Ubunifu wa hali ya juu.
Amesema,ni muda mrefu sasa kumekuwa na harakati mbalimbali za kuhamasisha utalii lakini Kwa Mkoa wa Dodoma juhudi zaidi Bado zinahitajika na kusema kuwa kupitia mbio hizo itasaidia watanzania kutilia mkazo mambo yote yanayohusu utalii na uhifadhi. .
Alisema Mkoa wa Dodoma una vivutio vingi vya kihistoria na kutolea mfano," hapa Kikuyu mbali na kuwepo kwa eneo la tembo,ukiingia ndani ya chuo kikuu cha St.Jonh kuna mti mkubwa uliotumika kunyongea wahalifu kipindi Cha utumwa lakini ukiwauliza wanaosoma pale hawajui chochote kuhusu mti huo,"amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Taasisi hiyo ya mtembezi Adventures, ambayo ndiyo waandaaji wakuu wa mbio za Mtembezi Samson Samwel amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mbio hizo zitachochea Utalii Dodoma.
Amefafanua kuwa mbio hizo zitafanyika tarehe 1 july ambapo kwa kuanza zitasindikizwa na Maonyesho ya siku tatu yatakayolenga kuonyesha utalii wa ndani Dodoma na Tanzania kwa ujumla na kwamba mbali na Dodoma zimefanyika katika mikoa mitatu tofauti yaani Dar Es Salaam,Kigoma na Tabora.
"Tulianza rasmi mwaka 2021 na tulipata umaarufu na kukua zaidi baada kwa kushindwa na aliekua mkuu wa wilaya ya Temeke wakati huo DC jokate mwigelo,tunajivunia kuwa na mafanikio zaidi,"anafafanua.
Mbali na hayo ameeleza kuwa Mtembezi Marathon ni mbio ambazo huandaliwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani nchini na kufanyika katika kanda na mikoa mbalimbali na kutangaza fursa za utalii zilizopo katika eneo husika.
Social Plugin