Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NICR YAELEZA MWELEKEO NA MAFANIKIO YAKE


Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NICR)imesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 hadi kufikia Juni 20 imesaini mikataba 48 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 234.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu na mabwawa yaumwagiliaji.

Aidha imesaini mikataba 22 yenye thamani ya shilingi Bilioni 25 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo mikataba mitatu kati ya hiyo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 23.9 kwa ajili ya ununuzi wa magari na mitambo.

Hayo yameelezwa leo Julai 28,2023 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NICR Raymond Mndolwa wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuwa tayari wamesaini hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni mbili kutoka nchi za Italia na Uispania kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu .

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni  kununua mitambo 15 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji,kununua magari 53 kwa ajili ya usimamizi wa miradi ya umwagiliaji na kupata fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia mradi wa PFoR ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2023/2024; Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 70 kwa miaka .

"Tume imefanikiwa kupata fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kupitia mradi wa “Irrigation Development Advisory”. Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024,"

Akielezea mwelekeo wa Tume hiyo, Mkurugenzi huyo wa NICR amesema ni kuendelea kutekeleza miradi itakayoongeza eneo la umwagiliaji lenye ukubwa hekta 256,185.46 ili kufikia hekta milioni 1,200,000 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020).

"Mwelekeo wetu mwingine ni huu wa awamu ya Tatu ya Mpango Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II) na kufikia hekta milioni 8.5 ifikapo 2030 (Agenda 10/30) ambapo ili kufikia malengo  tumepanga kutekeleza jumla ya miradi 822, ambapo miradi 114 ni ya ujenzi wa mabwawa na 103 ni ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji,"amesema 

Ameeleza kuwa,maeneo ya kipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 ni  Kukamilisha ujenzi wa skimu mpya 25 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023, kukamilisha ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 30 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023.

Hatua hiyo ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa mabwawa 14 yenye mita za ujazo 131,535,000 yaliyoanza kujengwa Mwaka 2022/2023, kukamilisha usanifu wa mabonde 22 ya Umwagiliaji ulioanza Mwaka 2022/2023.

"Lengo letu ni kufika mbali zaidi,tumeanza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mabonde 22 yenye jumla ya hekta 306,361, kuanza ujenzi wa skimu mpya 35 zenye jumla ya hekta 111,390 ikiwa ni pamoja na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji katika Skimu 24 zenye jumla ya hekta 32,092 na kufanya usanifu wa mabwawa mapya 100 yenye wastani wa mita za ujazo 936,535,700 na kuanza ujenzi wa mabwawa hayo,"amefafanua

Kuhusu kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya pamoja (Block farms), amesema  jumla ya hekta 79,518.46 katika Mikoa ya Kigoma, Njombe, Mbeya, Kagera na Dodoma kupitia programu ya Building Better Tomorrow (BBT) imeandaliwa .

Ili kutekeleza maeneo ya kipaumbele , Mndolwa amesema Tume imeidhinishiwa na Bunge kiasi cha Shilingi 373,511,998,000/= kwa ajili ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kwamba kati ya Fedha hizo, miradi ya maendeleo Shilingi 299,964,223,000 /= (80.3%) na matumizi ya Kawaida Shilingi 73,547,775,000 (19.7%).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com