Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. NOMBO AHIMIZA NACTVET KUSIMAMIA VYUO VYA MAFUNZO YA UFUNDI STADI


Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo leo tarehe 9 Juni 2023 ameitaka NACTVET kuongeza usimamizi wa vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kufikia ubora unaostahili.

Prof. Nombo ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa wamiliki wa vyuo binafsi vya Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayofanyika katika chuo cha Ualimu Morogoro.

Mafunzo hayo yamewaleta pamoja, wamiliki wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi Kanda za Kaskazini (Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara), Kanda ya Kati (Dodoma, Iringa, Singida) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Morogoro na Pwani). Malengo ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wamiliki wa Vyuo na Wakuu wa Vyuo hivyo kutoa mafunzo yanayokidhi viwango vya sasa kwa mahitaji ya soko la ajira.

“NACTVET ihakikishe kuwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi inatolewa kwa viwango na ubora unaohitajika na soko la ajira na hatimaye kuwa na wahitimu wenye ujuzi na umahiri”. Alisema Prof. Nombo.

Aliongeza kuwa, Serikali inathamini mchango wa vyuo katika kukuza ujuzi na umahiri na kuiagiza NACTVET itumie fursa hii kuendelea kukutana na wadau wa Mafunzo ya Ufundi Stadi kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzitatua kwa maendeleo ya nchi na uchumi endelevu.

Aidha, amevitaka vyuo kuandaa programu zenye tija na ubora unaokubalika kwani Serikali imewekeza katika miradi mbalimbali yenye kuhitaji wataalamu wenye ujuzi na umahiri katika kuendesha miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Prof. John Kondoro, alisema mafunzo haya yatawasaidia wamiliki na waendeshaji wa vyuo kufahamu sheria ,kanuni na taratibu za NACTVET katika kurekebu mafunzo ya ufundi stadi nchini pamoja na matarajio ya NACTVET kwa vyuo baada ya mafunzo haya.

Watumishi wa NACTVET wakiongozwa na Katibu Mtendaji Dkt. Adolf Rutayuga wameshiriki katika kutoa mafunzo hayo kulingana na idara pamoja na kurugenzi mbalimbali zilizo chini ya NACTVET. Miongoni mwao ni pamoja na Dkt. Alex Nkondola, Dkt. Amani Makota, Dkt, Jofrey Oleke na wakuu wa kanda husika - Dkt. Annastella Sigwejo (Mashariki), Dkt.Godfrey Komba (Kaskazini) na Bw. Ramadhani Samainda (Kati).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com