SERIKALI YAAGIZA MAENEO YOTE YENYE CHANGAMOTO YA KUWEKA NAMBA ZA NYUMBA NA MAJINA YA MITAA ZIKAMILISHWE


Na. Mwandishi Wetu

Serikali imeagiza kuwa maeneo yote yaliyokuwa na changamoto ya kuweka Namba za Nyumba na majina ya Mitaa yakamilishwe haraka ili zoezi hilo likamilike.

Hayo yamesemwa leo Juni 20, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Bw. Hashim Komba, wakati akifunga zoezi la Mafunzo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa na Watendaji Kata pamoja na wakusanya taarifa wa zoezi hilo yaliyofanyika Ukumbi wa La Dariot, Ubungo Mkoani Dar es salaam.

Mhe. Komba amesisitiza kuwa washiriki wote wahakikishe wanatoa ushirikiano wa kufanikisha zoezi hili kwa kuwa ni zoezi la muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu.

“Hakuna atakayekwamisha zoezi hili kwa sababu ni zoezi la kitaifa kwa maendeleo ya taifa letu, tutatatua changamoto zote ili kusiwe na pa kukwama katika zoezi hili” alisema Mhe. Komba

Akitoa salam kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Komba amesema kazi ya serikali ni kutatua changamoto zote zinazotatiza zoezi hili ili kuwawezesha wataalam kufanya kazi yao ya uhakiki, usasishaji na kuweka maboresho sehemu zitakazohitaji kufanya hivyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo (DAS), Ndgu Hassan Mkwawa amesema Umoja na Ushirikiano katika kazi hii ndiyo siri ya kufanikisha kwa haraka na kwa ufanisi zoezi hilo la Uhakiki wa Anwani za Makazi.

Aidha, Ndgu Mkwawa aliwaeleza washiriki kuwa zoezi hilo litachukua muda wa wiki moja na nusu kukamilika, hivyo wakati wote wa utekelezaji kunahitajika utashi, utimamu na nidhamu ya hali ya juu. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post