SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesaini Mikataba na Kampuni ya EAA iliyoshinda zabuni ya ukaguzi magari kutoka nchi ya Uingereza na Kampuni ya QISJ ambayo nayo ilishinda zabuni kukagua magari yanayotoka nchi za Falme za kiarabu yatakayoletwa nchini Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26,2023 wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt.Yusuph Ngenya amesema ukaguzi wa magari nje ya nchi kabla ya kuingia nchini itasaidia kuepusha gharama za matengenezo kwa mnunuzi kwani gari linapopimwa kabla ya kuwasili nchini, kasoro zozote zinazobainika kushughulikiwa huko huko kabla ya kuletwa nchini.
Amesema kuanzia mwezi Julai 2022, ukaguzi wa magari katika nchi ya Japan umekuwa ukifanywa na kampuni ya EAA ambayo ilishinda zabuni ya ukaguzi wa magari kutoka nchi hiyo yanayotarajiwa kuletwa hapa nchini.
Aidha amesema kampuni ya EAA pia imeshinda zabuni ya kufanya ukaguzi wa magari katika nchi ya Uingereza yanayotarajiwa kuletwa nchini Tanzania.
Pamoja na hayo amesema hivi karibuni kampuni ya QISJ imeshinda zabuni ya kukagua magari yanayotoka nchi za falme za kiarabu (UAE) yanayoletwa hapa nchini.
Hata hivyo amewataka wananchi wanaoagiza magari yaliyotumika kutoka nje ya nchi kuzingatia utaratibu wa kuhakikisha kuwa magari hayo yanakaguliwa kabla ya kuletwa nchini na kupata cheti cha kuthibitisha kukidhi matakwa ya viwango.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Kampuni ya EAA amesema watashirikiana na TBS kuhakikisha magari yanayoingizwa Tanzania yanakidhi viwango.
"Lengo letu ni kuwasaidia watanzania kupata magari bora, tunatamani wafurahie huduma zetu na kujivunia ubora wa magari yatakayoingizwa" amesema.