Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UONGOZI BANDARI ZA ZIWA VICTORIA WAFURAHIA MAFANIKIO,WAPONGEZA MABORESHO YALIYOFANYWA NA SERIKALI


Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Ferdinand Nyathi akiongea na waandishi wa habari akielezea utendaji kazi wa maboresho ya bandari hizo

***************

Na Mwandishi Wetu, Mwanza


MENEJA wa Bandari za Ziwa Victoria Ferdinand Nyathi ameelezea mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kwenye bandari hizo ikiwemo kuvuka lengo la kuhudumia shehena kwani mpaka Mei mwaka huu wameshahudumia jumla ya tani 246, 0000 ambazo ni sawa na asilimia 101.1.

Ameongeza kwa muda uliobakia upo uwezekana wa kuongezeka kiwango cha kuhudumia shehena lakini mafanikio mengine ni kuongezeka kwa mapato pamoja na meli zinazoingia kwenye bandari za Ziwa Victoria.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria Ferdinand Nyathi amefafanua mwaka wa fedha 2022/2023 bandari hizo ziliwekewa lengo la kuhudumia shehena tani 228,000 ambapo hadi kufikia Mei, mwaka huu jumla ya tani 246,000 zimeshahudumiwa.

"Bandari zetu zimefanya vizuri katika maeneo yote ikiwemo mapato, kuhudumia shehena na idadi ya meli zinazoingia katika bandari hizo, ", amesema na kuongeza kuhusu miradi yote ya maboresho katika bandari za Ziwa Victoria imelenga kuboresha maeneo yote ya bandari hizo.

Amesema kuwa maeneo yaliyoboreshwa ni kuongeza kina cha maji, maegesho ya meli, kuhudumia meli kubwa, miundombinu ya reli zinazoingia bandarini, majengo ya abiria, maeneo ya kuhifadhia mizigo, mifumo ya TEHAMA pamoja na mifumo ya ulinzi na usalama.

Pamoja na hayo ametoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea kutumia bandari za Ziwa Victoria kwani huduma zao ni nzuri, zimeboreshwa na wamekuwa wakitoa kipaumbele katika kuwasikiliza wafanyabiashara.

" Pia bandari zetu hivi sasa zinahudumia shehena ya mizigo inayokwenda bandari ya Kisumu jambo ambalo halikuwepo katika miaka miwili iliyopita.Tulikuwa hatupati mizigo inayokwenda bandari ya Kisumu,ila kuanzia mwaka huu wa fedha tumeanza kupata mizigo ya kwenda katika bandari hiyo.”

Amefafanua mizigo inayotoka na kwenda nchi jirani inachangia asilimia 50 ya mizigo yote inayohudumiwa katika bandari zetu za ziwa Victoria.

Kuhusu miradi inayotekelezwa kwa sasa, ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kutenga fedha kuboresha bandari za Ziwa Victoria huku akisisitiza tayari kuna miradi imeshaanza kutekelezwa katika bandari za Bukoba na Kemondo ikiwa thamani ya takribani sh bilioni 40”

Wakati huo huo mmoja wa Wakala wa Forodha Peter Zakayo amesema, wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka viongozi na watumishi wa bandari za ziwa Victoria huku akieleza pia huduma wanazopatiwa ni nzuri kwani hata mizigo hutolewa kwa wakati.
Mwonekano wa bandari za Mwanza Kusini na Mwanza Kaskazini ambazo ni miongoni mwa bandari za ziwa Victoria ikiwa ndio bandari kubwa zaidi.

 

Mhandisi Meli ambaye pia ni Kaimu Mhandisi Mkuu wa kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Mhandisi Abel Gwanafyo akiongea na waandishi wa habari kuhusu ujio wa meli kubwa itakayofanya kazi katika bandari za ziwa Victoria kufuatia miradi maboresho ya kuendeleza bandari hizo



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com