Serikali imewataka wadau wa Sekta ya Uchukuzi kwa njia ya maji Nchini kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani kujadili na kutafakari juu ya hali za mabaharia na mustakabali mwema wa ustawi wao katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa.
Hayo yamesemwa leo Juni 22,2023 na Mgeni rasmi Waziri wa Uchumu wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame wakati wa ufunguzi wa maonesho ya siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha vilivyopo katika Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza kuanzia Tarehe 22 mpaka 25 Juni,2023
“kazi ya ubaharia siyo uhuni ni kada yenye weledi wa kutosha na wataalamu mahili ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na Dunia kwani asilimia zaidi ya 80 ya mizigo na abiria husafirishwa kwa njia ya maji lakini wengi wao wanaendelea kuishi maisha magumu kutokana na mishahara duni, mazingira magumu ya kazi na kutokuwa na mapumziko wala likizo kwa mabaharia wanaoajiliwa na baadhi ya Wasafirishaji binafsi” amesisitiza Mhe. Makame
Mhe makame amesema Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mhe. Dkt Hussein Ally Mwinyi zimeweka kipaumbele kuwekeza katika miundombinu na vyombo vya usafiri majini kama vile ukarabati wa meli ya Mv Umoja ujenzi wa Meli mpya ya Mv mwanza bara na kuridhia ununuzi wa meli mbili mpya na ukarabati wa meli ya Mv mapinduzi kwa upande wa Zanzibar ambavyo vitasaidia kukuza ajira za mabaharia na kukuza uchumi huku zikihakikisha maslah ya mabaharia yanalidwa.
Mhe. Makame amewataka wadau wote wa sekta ya Uchukuzi kwa njia ya maji kutumia maadhimisho haya yanayofanyika Jijini Mwanza kujadili na kutoa mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuboresha maslah ya Mabaharia Nchini kwa maendeleo ya Taifa na Serikali ziko tayari kuyafanyia kazi.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Sekta ya Uchukuzi Bi.Stella Katondo amesema siku ya Mabaharia Duniani huazimishwa wiki ya mwisho ya mwezi wa sita kila mwaka Duniani kote na Nchi wanachama wa Shirika la Bahari Duniani(IMO) ambapo Tanzania ni Nchi mwanachama na kwa mwaka huu 2023 maadhimisho haya yanafanyika Kitaifa Jijini Mwanza.
Bi. Stella amesema Maadhimisho haya yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya Taasisi zinazojihusisha na masuala ya usafiri kwa njia ya maji,warsha ya wadau itakayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa, kufanya usafi katika mialo, kutoa elimu kwa wadau na Wanafunzi wa Vyuo, na zoezi la majaribio ya uokoaji inapotokea dharura majini.
“Maonesho haya yatahusisha wadau wote wa Sekta ya Uchukuzi kwa njia ya Maji ambapo watapata fursa ya kutangaza shughuli na majukumu yanayotekelezwa na taasisi zao,kutoa elimu ya uhamasishaji katika shule,vyuo,mialo pamoja na masoko ya samaki yaliyopo jijini mwanza” amesisitiza Bi. Stella
Awali akitoa salaam za Mkoa Naibu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Bi.Amina Makilagi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya Jiji la Mwanza ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR,Ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza na ukarabati wa meli ya Mv Umoja.
Mhe. Amina amesema Mwanza iko salama na kuzitaka Taasisi zote zinazoshiriki maadhimisho haya ya siku ya Mabaharia Duniani kutumia fursa hii pia kuangalia maeneo ya uwekezaji na kutembelea maeneo mbalimbali ya kitalii vikiwemo visiwa vya saa nane.
Maonesho ya siku ya Mabaharia Duniani yanayoanza tarehe 22 mpaka 25 Juni, 2023 yanayofanyika kitaifa Jijini Mwanza yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Sekta Uchukuzi kwa Tanzania Bara kupitia Shirika la uwakala wa Meli Tanzania(TASAC) na Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Zanzibar(ZMA), Pamoja na wadau mbalimbali wa Uchukuzi kwa njia ya maji Nchini.
Social Plugin