Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa kikao chake na Wapangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa wanaofanya biashara eneo la Kariakoo tarehe 19 Juni 2023.
****************
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewatuliza wapangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la kariakoo na kuwataka kufuata sheria na mikataba waliyoingia na shirika hilo.
Dkt Mabula amekuatana na wapangaji hao jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Juni 2023 kusikiliza kilio cha wapangaji hao waliotaka kuongezewa muda wa notisi ya miezi mitatu waliyopewa na NHC kupisha uwekezaji.
Aidha, wapangaji hao wameitaka serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa kuwapa kipaumbele cha kuwapangisha kwenye majengo wanayoishi na kuyatumia sasa mara mradi wa uboreshaji utakaofanywa na mbia kukamilika.
Kwa mujibu wa wapangaji hao wa eneo la Kariakoo, hawapingani na uwekezaji unaofanywa na serikali bali wanachotaka ni kushirikishwa, kuongezewa muda wa notisi sambamba kupewa kipaumbele cha kupangishwa pale mradi utakapokamilika.
Akijibu maombi ya wapangaji hao, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaambia wapangaji hao kuwa, katika suala la uendelezaji milki, Kariakoo ni eneo litakalofanyiwa maboresho makubwa na halitarudi katika hali yake ya sasa bali itakuwa na maboresho ya majengo.
Hata hivyo, amewaambia kuwa, hakuna mkataba uliosainiwa na mbia wala muundo wa majengo uliowekwa na Shirika la Nyumba la Taifa ambapo ameweka wazi kuwa wanaodai kupewa ubia na kuanza kukusanya fedha ni matapeli wanaotakiwa kuchukuliwa hatua.
‘’Kwanza nashangaa mtu kujiita mbia na kuanza kukusanya fedha hata kabla ya kuwa na uhakika unayekusanya pesa zake atakuwa mpangaji’’. Alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mkataba ulioingiwa baina ya Shirika la Nyumba la Taifa na Wapangaji una kila kitu na mpangaji anatakiwa kukijua ambapo aliwataka wanasheria wanaowashauri wateja wao kuhakikisha wanawashauri kwa kuzingatia mikataba badala ya kuwapa matumaini na kuleta taharuki.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wamesema hawapingani na serikali katika suala zima la ubia bali wanachotaka ni kupatiwa nafasi kutokana na maeneo kuwa machache na kuweka wazi kuwa kuhamishwa kwao haraka itawawia vigumu kupata nafasi maeneo mingine huku baadhi yao wakiwa na mikopo benki hivyo wameomba kuongezewa muda wa notisi.
‘’Sisi tuko na serikali na dhamira hawapingani na serikali na tumewakataza wale wote waliokuwa na dhamira tofauti na serikali katika kutafuta mbia wa kuwekeza kwenye eneo la kariakoo’’ walisema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah alisema, anachofurahishwa ni kwamba serikali na wapangaji wa eneo la kariakoo wanakubaliana na uendelezaji unaotaka kufanyika na tofauti ni namna ya eneo hilo linavyoendelezwa.
‘’Kwa kweli hapa nashukuru sana serikali na wapangaji wa eneo la kariakoo tuna dhana moja ya kukubali kariakoo kuendelezwa’’. Alisema Abdallah
Kufuatia maombi ya wapangaji hao, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula ameongeza muda wa notisi kutoka miezi mitatu hadi miezi sita ambapo sasa wapangaji hao watalazimika kupisha uboreshaji kufikia Desemba 31, mwaka huu na kusisitiza fursa iliyotolewa ni kwa wafanyabiashara wa kariakoo pekee na haitatumika kwa maeneo mengine ambayo ubia wa aina hiyo utafanyika.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) hivi karibuni lilingia katika sera ya ubia na watu binafsi sera yenye lengo la kuendeleza ama kuboresha majengo ya shirika hilo na kuyafanya kuwa ya kisasa na yenye muonekano wa kuvutia na hatimaye kuliongezea kipato shirika hilo.
Baadhi ya wapangaji wa NHC Kariakoo wakizungumza katika kikao chao na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula kuhusiana na uendelezaji wa majengo ya NHC kupitia sera ya ubia tarehe 19 Juni 2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga akizungumza katika kikao baina ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na wapangaji wa NHC eneo la Kariakoo tarehe 19 Juni 2023.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah akizungumza wakati kikao baina ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na wapangaji wa NHC eneo la Kariakoo tarehe 19 Juni 2023.
Baadhi ya wapangaji wa NHC wanaofanya biashara eneo la Kariakoo wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) walipokwenda kupeleka kilio chao kuhusiana na uendelezaji majengo ya shirika hilo kupitia sera ya ubia tarehe 19 Juni 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, akiwa katika picha ya pamoja na wapangaji wa NHC eneo la Kariakoo waliokwenda kuwasilisha maombi yao kuhusiana na uendelezaji wa majengo ya NHC kupitia sera ya ubia tarehe 19 Juni 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, akiagana na mmoja wa wapangaji wa NHC eneo la Kariakoo waliokwenda kuwasilisha maombi yao kuhusiana na uendelezaji majengo ya NHC kupitia sera ya ubia tarehe 19 Juni 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)