Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kutembelea maeneo ya utalii wa maporomoko ya maji ambayo yana historia kubwa ya utamaduni wa nchi yetu pia ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kufungamanisha utalii na utamaduni wa Taifa la Tanzania.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo alipotembelea leo maporomoko ya Mpanga Kipengere yaliyopo katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Njombe na kukagua shughuli mbalimbali za utalii na miundumbinu iliyojengwa na Mamlaka ya Wanyamapori Nchini (TAWA) kwa ajili ya kuhudumia wageni mbalimbali wanaotembelea maeneo hayo.
“Napenda kutoa wito kwa viongozi wa kuchaguliwa na wananchi na kuteuliwa kuwahimiza wananchi kuja kutembelea maeneo haya ili kuona urithi wa hazina ya utalii na utamaduni ambao haupatikani sehemu yoyote duniani isipokuwa katika maeneo hayo.”amefafanua Mhe. Mchengerwa
Amewataka watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye maeneo haya ambapo amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kutangaza maeneo yote yenye fursa za uwekezaji ili watu wenye uwezo wa kuwekeza waweze kuwekeza hatimaye kuliingizia taifa mapato.
Akizungumzia kuhusu maboresho ambayo Serikali inakwenda kufanya kwenye maporomoko ya Mpanga Kipengere kwa sasa ni pamoja na kujenga miundombinu ya kupumzikia wageni wageni, kuweka makasia na zip line.
Ameyataja maporomoko mengine ambayo ni sehemu ya Mpanga Kipengere kuwa ni pamoja na Kimani, Nyaugenge, Ikovo, Kipengere, Lyamakunohila na Nyaluliva ambayo kila moja lina aina ya utalii wa kipekee.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Joas Makwati wa Mpanga Kipengere amefafanua kuwa mbali ya kuwa eneo ni maarufu kwa maporomoko pia lina maua ya kipekee, safu za milima na Wanyama wa porini kama Mbuzi Mawe na toe.
Makwati amesema eneo hili ni miongoni mwa eneo mkakati kwa utalii nchini kutokana na eneo lililopo kijiografia ambapo amesema endapo juhudi za makusudi za kuleta wanyama zikifanyika zitasaidia kuwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kutembelea.
Aidha, amefafanua kuwa awali eneo hili lilikuwa na Wanyama wengi chini ya umiliki wa vijiji ambapo uwindaji haramu ulitamalaki hivyo kumalizika kwa Wanyama waliokuwepo.
Social Plugin