Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WASIRA AIVAA CHADEMA KWA UPOTOSHAJI WA BANDARI

* Awashutumu viongozi wa CHADEMA kuwa ni vibaraka wa mabeberu

* Asisitiza kuwa nchi wala bandari kamwe haziwezi kuuzwa

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira, ambaye alishiriki kwenye harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni mwaka 1961, amewashutumu vikali viongozi wa CHADEMA kwa kusambaza uongo kuwa nchi na bandari zimeuzwa, akisema kuwa chama hicho kinatumiwa na mabeberu kutaka kuvuruga uhuru, umoja, amani na utulivu nchini.

Akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mkoani Mbeya jana uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi, Wasira amesema kuwa uongo wa makusudi wa viongozi wa CHADEMA kuwa nchi na bandari zimeuzwa una lengo la kuzua taharuki kwenye taifa.

"Tukaambiwa nchi imeuzwa na bandari zote zimeuzwa. Kwa kweli wananchi walikuwa na haki ya kushangaa na kushtushwa na jambo hili. Sasa kama nchi imeuzwa, sisi ni mbuzi?" Alihoji Wasira.

 "Tukatoka kwenye hoja ya kuuza bandari tukaingia kwenye utaifa na ukabila, tukaingia na Uzanzibari na Utanganyika. Sasa ni bandari, ni Uzanzibari au ni Utanganyika?"

Wasira alionya kuwa watu waongo ni hatari kuliko watu wengine wowote kwenye jamii au taifa.

"Ukiuliza nchi au bandari imeuzwa kwa bei gani wanasema wameuza tu, maana hawana jibu. Nchi haiwezi kuuzwa, maana hatukudai uhuru wa kuuza," alisema Wasira, ambaye alikuwa kwenye TANU Youth League wakati wa harakati za kudai uhuru miaka 62 iliyopita.

"Mimi nimeonja ukoloni, nimeathiriwa na ukoloni na nilishiriki kudai uhuru. Unasema nchi yetu imeuzwa na uhuru wetu umeuzwa, halafu mimi nikae kimya?"

Wasira amesema kuwa kampuni binafsi yenye makao makuu Hong Kong, TICTS, iliendesha eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20 bila kelele zozote na akawashangaa wanaotaka kuzua taharuki kwa uamuzi wa Serikali kufanya majadiliano na kampuni ya DP World kuhusu uwekezaji mkataba wa kuendesha sehemu ya bandari ya Dar es Salaam, kama walivyopewa TICTS.

Kuhusu suala la usalama bandarini, alisisitiza kuwa eneo hilo nyeti la mipaka ya nchi litaendelea kuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi la Tanzania na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama zamani.

Alisema kuwa DP World inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwenye nchi zaidi ya 60 duniani, ikiwemo Uingereza, hivyo inaweza kuleta manufaa makubwa kwa Tanzania.

"Nchi yetu haiwezi kuuzwa chini ya CCM, labda kama ikiingia mikononi mwa vyama mawakala wa mabeberu ambao wanasema CCM imekaa muda mrefu sana. Na sisi tunauliza kwani tulikubaliana nao tukae muda gani?" Alisema.

"Inaonekana hatukuelewana. Tulivyowaambia tunataka kujitawala hatukusaini mkataba wa miaka. Tulisema tunataka kujitawala kwa sababu tunataka kuamua mambo yetu wenyewe."

Viongozi wakuu wa CHADEMA, ikiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika, wamekuwa wakipotosha kuwa bandari imeuzwa, lakini wameshindwa kutoa uthibitisho wowote kuwa bandari imeuzwa kwa Shilingi ngapi kwa mkataba upi wa mauzo.

Viongozi hao pia wamehusisha mjadala wa uwekezaji wa DP World na hoja ya Utanganyika na Uzanzibari, jambo ambalo Wasira amesema ni siasa za ubaguzi zenye lengo la kudhoofisha umoja na muungano wa Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com