Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameungana na Wananchi na Wafanyabiashara wa Kata ya Bugene wilayani Karagwe katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati mpya eneo la Kishao katika kata ya Bugene.
Bashungwa ameongoza harambee hiyo Leo tarehe 03 Julai 2023 iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya Karagwe na Ofisi ya Mbunge kwa kushirikia na Diwani wa Kata ya Bugene, Mhe.Mugisha Mathias.
Wakati akiongoza harambee hiyo, Bashungwa amechangia kiasi cha shilingi milioni 12 ambapo ameungwa mkono na Wananchi na wafanyabiashara wa kata Bugene kwa kuchangia jumla ya shilingi 37,635,000 na saruji mifuko 26
Bashungwa ametoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Karagwe kuunga Juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kujitoa kuchangia miradi ya maendeleo kama ilivyo kwa Wananchi wa Kata ya Bugene.
Aidha, Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa kuchangia shilingi milioni 80.4 zilizotumika katika ujenzi i wa shule ya Sekondari mpya ya Omurushaka ambapo Serikali ilitoa milioni 580 kuunga mkono Juhudi za wananchi ili kukamilisha shule hiyo ambayo tayari imeshapokea wanafunzi.
Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuelezea miradi mingi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika wilaya karagwe ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Jengo jipya la Halmashauri, Ujenzi wa ofisi mpya ya Mkuu wa wilaya na Ujenzi wa stendi mpya.
Katika Sekta ya Miundombinu, Bashungwa amezitaja barabara zinazoendelea kuimarishwa ili ziwezi kupitika misimu yote katika mwaka ambazo ni barabara ya Nyakayanja - Ihembe 1, barabara ya Ihembe 2 - Karehe Nyakahanga, barabara ya Ihembe-Kibogoizi na barabara ya Ruhita-Kibogoizi-Mato-Bujuruga-Miti-Kihanga.