SERIKALI YAANZA MCHAKATO WA UELIMISHAJI WA UMMA KUHUSU MAANDALIZI YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO

Na Mwandishi wetu - Kagera
Kuelekea ukomo wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, iliyoandaliwa mwaka 1999, Serikali imeanza mchakato wa uelimishaji wa umma kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.


Akifungua warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tarehe 21.07.2023, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa, amewataka wataalam kutumia fursa hii kufikiri zaidi, kuona nini kifanyike na namna ya kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera katika mpango ujao.


“Niombe Dira yetu iweke kipaumbele kwenye kuitazama Mikoa ambayo imeachwa nyuma kimaendeleo. Ijulikane wazi ni nini kinakwenda kufanyika ndani ya miaka 25 ijayo ili Mikoa hiyo itoke pale ilipo na ipande kiuchumi kama Mikoa mingine,” ameeleza Mhe. Hajjat Fatma.


Ameeleza kuwa Serikali lazima iwekeze rasilimali fedha za kutosha katika Mikoa iliyoachwa nyuma kimaendeleo na Halmashauri zake hazina mapato kwani mpango uliopo sasa kila Halmashauri inapanga Bajeti yake kulingana na pato lake la ndani. 

"Na fedha kutoka Serikali Kuu zinaelekezwa katika Miradi ya kimkakati na wizara husika. Ni mpango mzuri lakini una changamoto hivyo ni wakati sasa wa kuzingatia kuwa mapato ya Halmashauri yanatofautiana kuna Halmaahauri zina mapato makubwa na Halmashauri zingine zina mapato madogo hivyo kushindwa kutekeleza shughuli za maendeleo",amesema.


Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Nesphory Bwana ameeleza kuwa warsha hii ni maandalizi na kuwajengea uwezo viongozi watakaoshiriki katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandaa Dira ya Maendeleo ijayo ya mwaka 2050.


Amesema Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, ina nyenzo ya kuunganisha juhudi za Taifa katika kufikia malengo yanayotarajiwa ya kijamii na kiuchumi ili kuboresha hali ya maisha ya Mtanzania. Hivyo ni wakati sasa kila mmoja kutafakari kwa kina juu ya mafanikio ya Mpango huu uliopo na kwa yale ambayo hayakutekelezwa ni vema kuanza nayo, kuyapa kipaumbele na kuweka mikakati madhubuti wa namna bora ya kuyatekeleza.

Amesema ili kutimiza hayo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuboresha viashiria muhimu kama vile kuchochea ukuaji wa pato la Taifa na kushusha mfumuko wa bei, kuvutia wawekezaji kutoka nje, kupunguza ukosefu wa ajira pamoja na kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Mhandisi Omary Athumani Kiongozi wa Timu ya Uhamasishaji kutoka Wizara ya Fedha, ameeleza kuwa maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe umechukuliwa na utazingatiwa wakati wa kuandaa Dira hiyo ya mwaka 2050.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post