Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIKWETE: GGML WAMEONESHA NJIA UDHIBITI VVU, VIJANA JIHADHARINI



Rais mstaafu Jakaya Kikwete akimkabidhi bendera ya Tanzania Kiongozi wa msafara wa wapanda mlima Kilimanjaro, Henry Mazura (kulia). Rais Kikwete aliwaaga wapanda mlima 61 Julai 14 mwaka huu wanaoshiriki kampeni ya GGML KiliChallenge kwa lengo la kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TACAIDS, Jerome Kamwela.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Ummy Nderiananga (kulia) wakiwaaga wapanda mlima Kilimanjaro 61 wakiwamo 35 wanaouzunguka kwa baiskeli kupitia kampeni ya GGML KiliChallenge inayoratibiwa na kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na TACAIDS kwa lengo la kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi. Wapanda mlima hao waliagwa Julai 14 mwaka huu katika lango la Machame na wanatarajiwa kurejea Julai 20 mwaka huu katika lango la Mweka.

NA MWANDISHI WETU
RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuonesha njia katika kuunga mkono malengo ya Serikali kwenye mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kupitia Kampeni ya GGML Kili Challenge 2023.

Kampeni hiyo iliyoasisiwa na GGML mwaka 2002 kwa kushirikiana Taasisi ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) inalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi.

Aidha, akizungumza mwishoni mwa wiki Julai 14, 2023 katika hafla ya kuwaaga wapanda mlima 35 na waendesha baiskeli 26 watakaopanda Mlima Kilimanjaro kuhamasisha uchangishaji wa fedha hizo, Kikwete ametoa wito kwa vijana kujihadhari na ngono zembe.

Hafla hiyo ilifanyika katika lango la Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambapo wapanda mlima hao watapanda na kurejea tarehe 20 Julai mwaka huu.

Alisema ni dhahiri kuwa maambukizi ya VVU bado yapo licha ya kufikia asilimia 4.7 lakini ni vema Watanzania hususani vijana wakajihadhari na ngono zembe kwa kutumia kinga.

“Kama mnapanga siku na saa ya kukutana, usisahau kinga… unamwambia mwenzako wewe utaleta au mimi! tena kujihadhari chukua yako weka mfuko. Tusiache kukumbushana,” alisema.

Pia aliipongeza pia Serikali kwa kuendelea kuunga mkono mapambano hayo na kuongeza bajeti lakini akasisitiza fedha hizo hazitoshi hivyo ni vema wadau mbalimbali nao wakajitokeza kuunga mkono kampeni hiyo ambayo ni endelevu.

“Wanaopanda mlima Kilimanjaro ni mashujaa nawapongeza kwa kuwa mfano wa kuigwa. Niwatie moyo na kuwatakia kilala kheri kwani mmefanya uamuzi sahihi wa kishujaa wa kijitoa kwa ajili ya wengine hongereni sana” amesema.

Aidha, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong aliishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika kampeni hiyo.


Pia aliwatakia kilalakheri washiriki hao wanaopanda mlima Kilimanjaro na kuwaombea warejee salama.

Naye Kaimu Mkurugenzi Tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), Jerome Kamwela alisema wataendelea kushirikiana na GGML ili kuhakikisha ifikapo 2030 lengo la sifuri tatu linafikiwa.

Sifuri tatu maana yake kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Naye Naibu Waziri ofisi ya waziri mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Ummy Nderiananga alisema Serikali imeendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kwa kuongeza bajeti ya Mfuko wa Udhibiti wa Ukimwi (ATF) kutoka Sh bilioni 14 hadi bilioni 25.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema katika kuchangia kampeni hiyo mkoa huo umepanga kuchangia Sh milioni 51 na hadi sasa wamepokea fedha taslimu kutoka kwa wadau Sh milioni 31.


Aidha, Kiongozi wa Msafara wa wapanda mlima hao, Henry Mazura alisema wamejipanga kupanda mlima huo na kurejea salama.
Pia aliishukuru Serikali, GGML na wadau wengine kwa kuwatia moyo katika safari hiyo ngumu ikiwa ni ishara ya hamasa ya kukusanya fedha kwa ajili ya kampeni hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com