Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KOROSHO


Na Bryson Mshana - Mtwara

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Korosho utakaohusisha nchi 33 zinazolima zao la Korosho Duniani.


Mkutano huo ulioandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT unatarajiwa kufanyika Tarehe 11 October 2023 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC Jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya washiriki 500 kutoka katika mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki.


Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Mtwara Julai 14, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred, amezitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.


Ameeleza kuwa mkutano huo pia utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.


Bw. Francis amesema kuwa mkutano unakusudia kushirikisha wadau wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Korosho kama vile wakulima, wabanguaji, wasindikaji, wakaangaji, wasafirishaji na Vyama vya Ushirika.


Wengine watakaoshirikishwa ni Wasambazaji wa pembejeo, waendesha ghala, watafiti, wazalishaji wa mitambo na vipuli, wasimamizi wa Tasnia, walaji au watumiaji wa bidhaa za korosho, Taasisi za fedha, watunga sera, wawekezaji, wabia wa maendeleo na wadau wengine wengi.


“Bodi ya Korosho Tanzania inaandaa Mkutano huu wa kimataifa wa Korosho wenye wazo kuu la fursa za uwekezaji kwenye tasnia ya Korosho Tanzania (an insight and investment opportunities in Cashew Industry Tanzania) na kauli mbiu ni “wekeza kwenye Korosho kwa mendeleo endelevu” (invest in cashew for sustainable development).


“Mkutano huu unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo tunategemea kupata uwekezaji wa kwenye 2 mashamba makubwa, Ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi”,ameeleza Francis.


Bodi ya Korosho Tanzania imeandaa fomu ya kidigitali iliyoko kwenye tovuti ya Bodi ya Korosho Tanzania (www.cashew.go.tz) ambayo itatumiwa na washiriki kuomba kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wa mwaka 2023.


Aidha, washiriki wa ndani ya nchi wataweza kupiga namba ya bure ya Bodi 0800112159 ili kupewa maelekezo ya namna ya kujisali pale watakapokuwa na changamoto kwenye kujaza fomu, sambamba na fomu za usajili zitakazopatikana kwenye ofisi za Bodi zilizoko Mtwara, Dar es Salaam, Tanga, Tunduru, Manyoni na Morogoro ambazo mshiriki atajaza na kuziacha ofisini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com