Kijana Simoni Nyamsika (30) ambaye aliripotiwa kujikata sehemu za siri Mkoani Lindi, anaendelea vizuri kiafya baada ya kupatiwa matibabu ya haraka katika Hospitali ya Rufaa Sokoine Mkoani Lindi huku maelezo ya Daktari yakisema, itakuwa vigumu kwake kushiriki tendo la ndoa japo anaweza kuzalisha kupitia njia za kitaalamu.
Kijana huyo alitekeleza tukio hilo baada ya kupata changamoto ya Afya ya Akili, ambapo inaelezwa alifanya tukio hilo nyumbani kwake na kukimbilia Baharini kwa dhumuni la kujiosha ndipo wasamaria walipomsaidia kufika kituo cha Polisi na Baadae Hospitali kwaajili ya Matibabu.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sokoine Dr Baraka Steven amesema, kijana huyo baada ya kupata fahamu alizungumza na wataalamu wa saikolojia na Afya ya akili na kukiri kujikata uume wake kwa kutumia kisu huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo kumetokana na agizo kutoka juu, Agizo ambalo hadi sasa halijafahamika.
Mfawidhi anasema, Hali ya Mgonjwa kwa sasa ni nzuri kiafya kwani wamefanikiwa kumweka sawa katika eneo lake la uume huku suala la kijana huyo kuweza kushiriki tendo la ndoa likitajwa kuwa ni changamoto.
"Alikiri kujikata akisema ni agizo kutoka juu, tumefanikiwa kutibu jeraha lake japo kwa sasa itakuwa ngumu kwake kushiriki tendo la Ndoa" Dr Baraka Steven, Mganga Mfawidhi.
Chanzo _ EastAfricaTV