Sekta ya Madini imekuwa miongoni mwa Sekta zilizopata nafasi ya kunadi fursa zake za uwekezaji kwa ujumbe wa Wawekezaji kutoka Jimbo la Haryana nchini India.
Ujumbe huo wa wawekezaji takribani 150 unashiriki katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara SabaSaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akitoa wasilisho kuhusu Sekta ya Madini nchini na fursa zilizopo, Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wizara ya Madini Veronica Nangale ameelezea fursa ambazo wawekezaji hao wanaweza kushirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na utafiti wa madini, uchimbaji, biashara ya madini, uongezaji thamani madini na miradi ya ubia kupitia Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) na kampuni nyingine za ndani.
Veronica ameeleza kuhusu utajiri ambao nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nao na kuongeza kwamba, zipo fursa nyingi katika sekta ya madini ambayo nchi hiyo inaweza kuzitumia suala ambalo litaongeza ushirikiano ambao nchi hizo mbili zimekua nao kwa miaka mingi.
Baada ya wasilisho hilo na mengine, wawekezaji hao wamepata nafasi ya kukutana ana kwa ana na wataalam wa sekta zilizotoa mada ili kupata taarifa zaidi za kina na kukaribishwa kutembelea banda la madini kukutana na wadau wengine wanaoshiriki maonesho katika banda hilo.
Wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika madini ya phosphate, quarz, colbat, lithium, mawe ya nakshi na baadhi wakitaka kupata taarifa zaidi kuhusu miradi ya ubia.
Sekta nyingine zilizotoa wasilisho katika Siku hiyo ya India ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Wakala wa Misitu Tanzania(TFS), EPZA na ZPA.
Jukwaa hilo limelenga kujenga mahusiano na ushirikiano wa kibishara, kiuwekezaji kati ya Tanzania na India.