Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI AKAGUA MIRADI YA MAJI WILAYANI SHINYANGA, ATOA MAAGIZO KWA MKANDARASI ANAYETEKELEZA MRADI WA TINDE


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akikagua mradi wa tanki la kuhifadhia maji lililopo Kata ya Tinde.

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji nchini Mhandisi Cyprian Luhemeja amefanya ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maji wilayani Shinyanga.

Ziara hiyo imefanyika jana Julai 21, 2023 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga yenye lengo la kukagua ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji, uendeshaji wa mamlaka za maji na ubora wa utoaji wa huduma kwa wateja mkoani Shinyanga.

Ziara hiyo iliohusisha kutembelea miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa tanki la kuhifadhia maji kutoka ziwa Victoria uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 24.4 utakaowanufaisha wakazi zaidi ya laki moja vikiwemo vijiji 22 vya kata ya Tinde, mradi wa tanki la maji uliopo Ishinabulandi, pamoja na mradi wa maji ya ziwa Victoria katika shule ya msingi Bulambila na mradi wa maji kata ya Mwalukwa iliyofadhiliwa na wadau wa maendeleo LIFEWATER INTERNATIONAL .

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja, ametoa maagizo kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza kazi ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji 22 katika Mradi wa Maji Tinde wilayani Shinyanga hadi kufikia mwezi Agosti aanze kazi mara moja.

“Mradi huu umekwisha kamilika kwa asilimia kubwa na tayari fedha za kusambaza huduma ya maji kwa wananchi zipo, Mkurugenzi wa SHUWASA na kuelekeza wasiliana na Meneja Mradi ili Mkandarasi ambaye anayetekeleza mradi huu aanze kusambaza huduma ya maji kwa wananchi hadi kufikia mwezi Agosti awe ameshaanza kazi mara moja na kuvifikia vijiji vyote 22,”amesema Mhandisi Luhemeja.

Mkurugenzi wa Shirika la LIFEWATER INTERNATIONAL Revocatus Kamala amesema kuwa wanatarajia kuwa na vituo vya maji 28 kwenye kata ya Mwalukwa ambapo mpaka sasa vituo 7 tayari vimeanza kufanya kazi.

“Sisi kama shirika tunajihusisha na masuala ya maji na usafi wa mazingira ambapo mpaka sasa tuna kaya zaidi ya asilimia 90 zenye vyoo bora tunashukuru wizara imeendelea kutupa ushirikiano, shughuli hii ya mradi wa maji kwenye eneo hili tumetekeleza kwa kushirikiana na RUWASA kwa kupeana miongozo na wataalamu ili kufanikisha jambo hili”, amesema Kamala.


Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Bulambila Mwalimu Pius James amesema ya kukamilika kwa mradi huo wa maji shuleni hapo umekuwa msaada mkubwa na kuondoa changamoto ya uhaba wa maji na kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa hawaendi shuleni hivyo.

“Hapo awali tulikuwa na matundu mawili ya vyoo hapa shuleni huku upatikanaji wa maji ulikuwa bado ni changamoto lakini mara baada ya kukamilika kwa mradi huo wa maji safi na salama pamoja na vyoo bora ni matarajio yetu kuwa tutakwenda kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kwa sababu uwepo wa maji safi shuleni kumepunguza utoro wa wanafunzi, niwashukuru wadau wa LIFEWATER INTERNATIONAL pamoja na viongozi wa serikali kwa jitihada hizi”, amesema Mwalimu Pius.

Mbunge wa jimbo la Solwa Ahamed Salum amesema kipaumbele kikubwa cha utekelezaji wa miradi ya maji ya ziwa Victoria kwenye jimbo hilo ni katika taasisi zate za serikali ikiwemo vituo vya afya, zahanati pamoja na shule za sekondari na msingi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza mara baada ya kutembelea mradi wa huduma ya maji kwenye shule ya msingi Bulambila.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na menejimenti ya SHUWASA kwenye mradi wa maji tanki la Tinde.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja akikagua mradi wa tanki la kuhifadhia maji lililopo Kata ya Tinde.
Mradi wa tanki la kuhifadhia maji lililopo kata ya Mwalukwa wilayani Shinyanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja,(kulia) akiwa na Mbunge wa Solwa Ahmes Salum, wakimtwisha Ndoo ya Maji Mwanamke mkazi wa Mwalukwa wilayani Shinyanga katika ziara ya kukagua miradi ya maji.
Mradi wa maji ya ziwa victoria uliopo kwenye shule ya Bulambila.
Mradi wa vyoo bora uliojengwa katika shule ya msingi Bulambila.
Mradi wa maji Ishinabulandi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com